TFF yasusha viingilio Uwanja wa Chamazi-AZAM

Rais wa TFF, Leodger Tenga

*Simba Vs Villa waingiza mil 30/-

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanyia marekebisho viingilio vya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zitakazochezwa katika Uwanja wa Azam ulioko eneo la Chamazi, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi za uwanja huo sasa vitakuwa sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 kwa jukwaa kuu badala ya vile vya awali vya sh. 3,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa kuu. Mabadiliko hayo yalianza kwenye mechi ya jana kati ya Azam na JKT Oljoro.

Hata hivyo, viingilio hivyo havitatumika kwa mechi zitakazohusu mechi ambazo timu za Simba na Yanga zitacheza kwenye uwanja huo.

Wakati huo huo, mechi namba 107 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Villa Squad na Simba iliyochezwa Februari 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 30,017,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo ni 8,698 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B na sh. 15,000 VIP A.

Baada ya kuondoa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,578,864.41 fedha zilizobaki zilikuwa sh. 25,438,135.59. Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000.

Posho ya kujikimu kwa mwamuzi wa akiba sh. 30,000, gharama za tiketi sh. 3,960,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000. Nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 608,860 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 521,880.

Mgawo baada ya gharama za awali; uwanja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kila moja ilipata sh. 1,503,853.56, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 751,926.78, gharama za mechi sh. 1,503,853.56, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 150,385.36, DRFA sh. 601,541.42 na kila klabu ilipata sh. 4,511,560.68.