TFF Yapokea Maombi ya Kagame CUP 2015

TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TF, leo hii limepokea maombi toka Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), likiitaka Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ngazi ya vilabu yatakayotimua vumbi kuanzia mwezi Julai mwaka huu.

Kufuatia maombi hayo ya uenyeji wa michuano ya CECAFA kwa ngazi za vilabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame CUP), TFF inatafakari juu ya maombi hayo na itayatolea maamuzi.

SEMINA YA MAKOCHA WAKUFUNZI
Semina ya Makocha wakufunzi inatarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam kuanzia Aprili 27, 2015 na kumalizika Mei 2 Mwaka huu ikiwajumuisha jumla ya makocha wakufunzi 21.

Watakaohudhuria semina hiyo na leseni zao kwenye mabano ni; Michael Bundala (A) Ilala, Leodgar Tenga (A) Kinondoni, George Komba (A) Dodoma, Don Korosso (A) Kyela-Mbeya, Wilfred Kidao (B) Ilala, Rogasian Kaijage (A) Mwanza, Mkisi Samson (B) Mbeya, Dr. Mshindo Msolla (A) Kinondoni, Ally Mtumwa (A) Arusha, Madaraka Bendera (A) Arusha.

Wengine ni Juma Nsanya (A) Tabora, Hamim Mawazo (A) Mtwara, Wanne Mkisi (B) Kinondoni, Major Abdul Mingange (A) Kinondoni, Dr. Jonas Tiboroha (C) Ilala, Nasra Mohamed (A) Zanzibar, John Simkoko (B) Morogoro, Juma Mgunda (B) Tanga, Triphonia Temba (B) Manyara, Ambonisye Florence (C) Pwani, na Eugen Mwasamaki (B) Dar es salaam.

VPL KUENDELEA KESHO
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea kesho jumanne kwa mchezo mmoja katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, vinara wa ligi hiyo Young Africans watawakaribisha timu ya Stand United kutoka mjini Shinyanga.

Ligi hiyo itaendelea siku ya jumatano kwa michezo miwili, Simba SC watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku Polisi Morogoro wakiwakaribisha Coastal Union katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.