BAADA ya Libya kujitoa kuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika (AFCON) za 2017, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limealika nchi wanachama kuomba uenyeji wa fainali hizo. Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Agosti 24 mwaka huu) imeamua Tanzania kuomba uenyeji wa fainali hizo.
Tunatambua kuwa moja ya masharti ya kuandaa fainali hizo ni pamoja na nchi kuwa imeandaa moja ya mashindano ya vijana. Lakini kwa kuwa suala hili liko katika mazingira maalumu (exceptional circumstances) tunaamini CAF watafikiria ombi letu kwa msingi huo. Awali Libya ilipewa uenyeji wa fainali hizo 2015, lakini zikahamishiwa Afrika Kusini kutokana na sababu za kiusalama. Hivyo, Libya ikapewa fainali za 2017 ambapo sasa imejitoa yenyewe kuandaa fainali hizo.
BONIFACE WAMBURA MKURUGENZI MPYA WA MASHINDANO TFF
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemteua Boniface Wambura kuwa Mkurugenzi mpya wa Mashindano kuanzia Septemba 1 mwaka huu. Kabla ya uteuzi huo, Wambura alikuwa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF kuanzia Januari 1, 2011. Nafasi hiyo sasa iko wazi na itajazwa baadaye na Kamati ya Utendaji. Kamati ya Utendaji ya TFF inamtakia kila la kheri Wambura katika wadhifa wake huo mpya.
RUSHWA NA KUPANGA MATOKEO
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeamua kuanzia sasa adhabu kwa watu wanaotoa rushwa au kupanga matokeo katika mpira wa miguu kuwa ni kufungiwa maisha kujishughulisha na mchezo huo.
NOOIJ AITA 26 STARS KUIKABILI MOROCCO
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza kikosi cha wachezaji 26 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya FIFA Date dhidi ya Morocco itakayochezwa Septemba 5 mwaka huu nchini Morocco. Wachezaji walioitwa ni makipa Deogratias Munishi (Yanga) na Mwadini Ali (Azam). Mabeki ni Said Morad (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Shomari Kapombe (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Azam), Aggrey Morris (Azam), Joram Mgeveke (Simba) na Charles Edward (Yanga).
Viungo ni Erasto Nyoni (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Amri Kiemba (Simba), Himid Mao (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Ndemla (Simba), Said Juma (Yanga) na Haruna Chanongo (Simba).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Khamis Mcha (Azam), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngassa (Yanga), Mwegane Yeya (Mbeya City) na Juma Liuzio 9ZESCO, Zambia). Timu hiyo itaingia kambini Jumapili (Agosti 31 mwaka huu) mchana katika hoteli ya Accomondia.
Mwesigwa Selestine
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)