SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linampongeza Amani Ibrahim Makungu kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uchaguzi uliofanyika Juni 30 mwaka huu kwenye hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar.
Ushindi wa asilimia 94 alioupata Makungu ambaye hakuwa na mpinzani katika uchaguzi huo mdogo unaonesha imani ambayo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA wanayo kwake katika kukiongoza chama hicho.
Ni matarajio ya TFF kuwa ushindi huo utatafsiriwa kwa vitendo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA na wadau wa mpira wa miguu Zanzibar kwa kumpa Makungu ushirikiano wa asilimia 100 ili kuhakikisha Kamati yake ya utendaji inafanya kile kinachotarajiwa na wengi.
Makungu si mgeni katika mpira wa miguu, na mchango aliotoa kwa mchezo huo visiwani kabla ya kuwania nafasi hiyo unatambuliwa na kila anayefuatilia maendeleo ya mpira wa miguu katika Zanzibar.
TFF tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ZFA chini ya Makungu kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Ali Ferej Tamim ili kuhakikisha ustawi wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.