*Twiga Stars Zimbabwe kukipiga kesho
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mhariri wa Michezo wa gazeti la Mtanzania, Rachel Mwiligwa kilichotokea Mei 11 mwaka huu katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Rachel kwa kipindi chote akiwa mwandishi na baadaye Mhariri alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Rachel, kampuni ya New Habari ambayo ndiyo inayomiliki gazeti za Mtanzania na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Rachel mahali pema peponi. Amina
Wakati huo huo; timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) na Zimbabwe zinapambana kesho Mei 12 mwaka huu katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars ambayo ilikuwa katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza imerejea leo (Mei 11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam tayari kuikabili Zimbabwe. Ikiwa Mwanza jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi Rock City Queens, lakini mechi hiyo ilivunjika dakika ya 58 kutokana na mvua kubwa. Hadi mechi inavunjika, Twiga Stars ilikuwa ikiongoza kwa mabao 5-0.
Kwa mujibu wa kocha wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa, mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi ya mashindano ya Afrika (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi hiyo itachezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya kurudiana Dar es Salaam wiki mbili baadaye.
Naye Kocha wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza amesema amefurahi kupata mechi hiyo kwa vile anaamini Twiga Stars ni kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi yao ya AWC dhidi ya Nigeria.
Twiga Stars na Zimbabwe zilishakutana mara mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.
Mechi ya pili ilikuwa michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba kuanzia saa 10.30 jioni ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.