TFF yamlilia mchezaji Rashid Moyo

Rashid Moyo

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa, Rashid Moyo kilichotokea usiku wa Desemba 25 mwaka huu kwao Msambweni, Tanga.

TFF imesema hayo leo katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura. Katika taarifa hiyo Wambura amesema Moyo ambaye aliichezea timu ya Taifa kwenye miaka ya 70 alizikwa Desemba 26 mwaka huu kwenye makaburi ya Mabawa mkoani Tanga. Pia alikuwa mchezaji wa timu ya Coastal Union ya mkoa wa Tanga.

Amesema msiba huo ni pigo kwa familia ya Moyo, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati akiwa mchezaji.

Aidha Wambura ameongeza kuwa TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Moyo, Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tanga (TRFA) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 100,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
Mungu aiweke roho ya marehemu Rashid Moyo mahali pema peponi. Amina