TFF yamlilia marehemu Msafiri Mkeremi

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa kimataifa Msafiri Mkeremi kilichotokea alfajiri ya Agosti 2 mwaka huu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.

Licha ya kuwa mwamuzi, Mkeremi aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) sasa TFF kwa vipindi viwili tofauti. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT).

Vilevile aliwahi kuwa mkufunzi wa waamuzi, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Pwani.
Kwa upande wa vyama vya mpira wa miguu aliwahi kuwa kiongozi katika mikoa ya Tabora, Pwani na wilayani Mpanda katika Mkoa wa Rukwa.

Msiba wa Mkeremi uko nyumbani kwake Urambo, na kwa mujibu wa mtoto wake Masoud Mkeremi, atazikwa Jumamosi kwenye makaburi ya Msafa yaliyoko wilayani Urambo.

TFF inatoa pole kwa familia na kuitaka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Marehemu aliyekuwa akisumbuliwa na presha na ugonjwa wa kisukari ameacha wajane wawili na watoto 12. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina