TFF Yaifuata CRDB, Yafanya Marekebisho ya Katiba

Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Desemba 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam, imezingatia upungufu uliopo katika utekelezaji wa matumizi ya tiketi za elektroniki.
 
Hivyo, Kamati hiyo imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na benki ya CRDB inayoendesha mfumo huo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kuhusu upungufu huo na kuhakikisha unafanyiwa kazi.
 
MAREKEBISHO YA KATIBA YA TFF
Kamati ya Utendaji ya TFF imerejea mazungumzo kati yake na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwa nchini ukiongozwa na Meneja wa Vyama Wanachama wa FIFA, James Johnson.  
 
Mazungumzo hayo kuhusu Katiba ya TFF yalifanyika Desemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kamati ya Utendaji inasubiri rasimu ya Katiba hiyo kutoka FIFA ili iweze kufanya utaratibu wa kuwaarifu wanachama wake juu ya maudhui ya rasimu hiyo.
 
Shughuli ya FIFA kurekebisha katiba za nchi wanachama wake inaendelea duniani kote, na kwa Afrika kazi hiyo imekamilika katika nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi.
 
USHIRIKIANO KATI YA TFF NA SAFA
Kamati ya Utendaji imepitia na kupitisha makubaliano ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA). Makubaliano hayo ni ushirikiano katika nyanja za mpira wa miguu wa vijana, maendeleo ya waamuzi, ufundi, menejimenti ya matukio (event management) na utafutaji udhamini (sponsorship).
 
KANUNI ZA LESENI ZA KLABU (CLUB LICENSING REGULATIONS)
Kamati ya Utendaji imejadili rasimu ya Kanuni za Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations), na kuagiza Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ifanye marekebisho ya mwisho, kabla ya kanuni hizo kusainiwa na kuanza kutumika.