Na Joachim Mushi
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) imefuta uchaguzi wa Chama Cha Soka Mkoani Dar es Salaam (DRFA) uliokuwa ufanyike Machi 18, 2012. Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa mtandao huu kutoka TFF na kusainiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Deogratias Lyatto baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo imetoa maelekezo kwa DRFA ambayo inatakiwa yafanyiwe kazi kabla ya kufanya uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo miongoni mwa maelekezo ni pamoja na DRFA kufanya marekebisho katika baadhi ya vifungu vya katiba yake ambavyo vinakinzana na Mamlaka ya Katiba ya TFF kwa maelekezo ya Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezajia.
“Kutokana na mapungufu ya msingi katika Ibara ya 29, na Ibara ya 30 katika Katiba ya DRFA Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Katiba ya DRFA Ibara ya 48 na Kanuzi za Uchaguzi kwa wanachama wa TFF Ibara ya 26(2) Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kutumia mamlaka yake Kikatiba na Kanuni imefuta uchaguzi wa DRFA.
Hata hivyo imeeleza viongozi wa sasa wataendelea kuwa madarakani hadi hapo uchaguzi utakapofanyika tena ikiwa ni kabla ya Agosti 10, 2012, ambapo marekebisho yote yatakuwa tayari.
Wakati huo huo, taarifa ya jumla iliyotolewa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Februari 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kufanya uamuzi kwa ajenda mbalimbali ikiwemo Marekebisho ya Katiba za Wanachama wa TFF, na pia ushauri wa kisheria ulioombwa kwake na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Uamuzi uliofanywa kwa wanachama wote 40 wa TFF ni ufuatao; wanachama wote wanatakiwa kufanya marekebisho kwenye katiba zao katika maeneo matatu kwa mujibu wa maelekezo ambayo TFF ilitoa mwaka jana.
Maeneo hayo ni sifa za wagombea uongozi ambapo kwenye kipengele cha elimu ni lazima iwe kuanzia kidato cha nne, kutopeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za kawaida na kamati zao za uchaguzi kufanya kazi chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Hivyo hakuna mwanachama yeyote wa TFF anayeruhusiwa kufanya uchaguzi kwa sasa kama katiba yake ina upungufu au inakwenda kinyume na maelekezo kuhusu maeneo hayo matatu.
Kamati imetoa hadi Juni Mosi mwaka huu kwa wanachama ambao katiba zao zina upungufu katika maeneo hayo wawe wamefanya marekebisho ndiyo waendelee na uchaguzi kwa wale ambao muda wa uchaguzi umefika.
Ushauri wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni kuwa katiba zote za wanachama ziwe na vitu hivyo vitatu.