TFF yafanya marekebisho ratiba ya VPL

KOMBE LA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya marekebisho madogo kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kupisha mechi mbili za Taifa Stars zinazotarajiwa kuchezwa Februari 23 na 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo itafanyika Februari 23 mwaka huu wakati ile ya mashindano dhidi ya Msumbiji itachezwa Februari 29 mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo leo Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Bonifasi Wambura amesema marekebisho hayo yamefanywa kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kuwa pale ambapo Taifa Stars itakuwa na mechi, ligi itasimama kupisha mechi husika.

Amesema tarehe mpya za mechi husika na namba zake ni kama ifuatavyo; mechi namba 131 kati ya JKT Ruvu na Toto Africans sasa itachezwa Machi 3 mwaka huu, mechi namba 132 kati ya Yanga na Azam (Machi 10 mwaka huu), mechi namba 133 kati ya JKT Oljoro na Kagera Sugar (Machi 3 mwaka huu).

Wambura ameongeza kuwa mechi namba 134 kati ya Polisi Dodoma na Kagera Sugar (Machi 11 mwaka huu), mechi namba 135 kati ya Moro United na JKT Ruvu (Machi 3 mwaka huu), mechi namba 136 kati ya African Lyon na Ruvu Shooting (Machi 7 mwaka huu) na mechi namba 137 kati ya JKT Oljoro na Toto Africans (Machi 7 mwaka huu). Timu zilizotajwa mwanzo ndizo zitakazokuwa zinacheza kwenye viwanja vyake vya nyumbani.