Na Mwandishi Wetu
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea wikiendi hii kwa mechi tatu zitakazokutanisha timu sita kwenye viwanja tofauti.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Azam katika mechi itakayochezwa Machi 10 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Machi 11 mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Simba na Toto Africans ya Mwanza itakayochezwa kwenye uwanja huo huo.
Viingilio katika mechi hizo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 15,000.
Mechi nyingine itakayochezwa Machi 11 mwaka huu itakuwa kati ya Polisi Dodoma na Kagera Sugar. Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Jumatano ya Machi 14 mwaka huu kutakuwa na mechi mbili. Simba watakuwa wageni wa Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma wakati Yanga watakuwa wenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
wakati huo huo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangala anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kuchangia timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kupitia Tigo Pesa.
Uzinduzi huo wa akaunti maalumu ya Twiga Stars kupitia mtandao wa Tigo utafanyika kesho (Machi 10 mwaka huu) saa 5 kamili asubuhi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na unafanywa chini ya uratibu wa kampuni ya Edge Entertainment.
Twiga Stars iko kwenye mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini Addis Ababa.