SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa habari Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea Novemba 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Wakati TFF ikitoa tamko la rambirambi waandishi wa habari mbalimbali wameoneshwa kuguswa na kifo cha ghafla cha mwanahabari Mnyuku pamoja na kile cha mwanahabari Karashani kilichotokea akipatiwa matibabu juzi katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi Lugalo ya jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wao TFF wamesema, msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu nchini kupitia kalamu zao.
“Munyuku alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kampuni ya New Habari 1996 akiripoti habari za mpira wa miguu. Tunatoa pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), na kampuni ya New Habari 1996 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe,” ilisema taarifa hiyo ya TFF.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Daraja wachapishaji wa Gazeti la Kwanza Jamii, aliandika katika mtandao wa kijamii kuwa; “Nimekuwa na Munyuku muda mrefu…ndani ya tasnia na kwenye maisha ya kawaida changanyikeni, wanakoishi na kufanya shuguli zao watu wanaoitwa wa kawaida. Hakupenda makuu. Hakudharau mtu. Alipenda ucheshi hata kwa watu asiowatambua. Atangulie na akapumzike kwa amani ikiwa huo ndiyo wigo wa Kazi na maisha yake duniani. Mbele yake nyuma yetu kamanda.”
Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, wachapishaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo aliandika katika mtandao wa jamii; “Mungu aipumzishe mahali pema roho ya mwanahabari mwenzetu Innocent Munyuku. Awajalie wana familia moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.”
Naye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile akionesha kuguswa na msiba wa Mnyuku aliandika kwenye mtandao wa Jamii; “…Jamani, yapo mambo unashindwa kuamini iwapo yametokea kweli. Kwamba Munyuku amefariki, inaniingia akilini kwa tabu kidogo. Sisi tu waja wake yatupasa tujiandae kwani hatujui siku wala saa atakapokuja Mwana wa Mungi.
Taarifa za awali toka kwa marafiki wa karibu wa Mnyuku na wafanyakazi wenzake zinasema alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo na amewahi kulazwa mara kadhaa hospitalini. Hata hivyo kifo chake kimetokea akiwa usingizini; na hakika hakuwa amelalamika kabla kusumbuliwa na ugonjwa wowote.
Mwanahabari mkongwe Joe Beda ambaye anafanya kazi na Mnyuku alisema Ibada ya kumuaga itafanyika Jijini Dar es Salaam Ijumaa baadaye atasafirishwa kwenda kwao, Mzumbe, Morogoro kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumamosi.