Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea leo alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ajali ya gari Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri uwanjani.
Wakati mauti inamkuta, Mafisango alikuwa ameitwa Amavubi kwa ajili ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika zinazochezwa mapema mwezi ujao.
TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi. Amina