TFF, Serikali Waipongeza Taifa Stars, Mechi Yavuna Mil 226/-

Rais wa TFF, Leodger Tenga

MECHI ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na
Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jana (Machi 24 mwaka huu) na
Stars kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 226,546,000.

Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi
kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh.
10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo
sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh.
8,625,641.88.

Nyingine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia
15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh.
25,222,854.67 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) sh. 6,305,713.67.

Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh.
71,885,135.82 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.

TENGA AWAPONGEZA WACHEZAJI, SERIKALI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
ameipongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi,
washabiki, mdhamini na Serikali kwa kufanikisha ushindi wa jana.

Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau
wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na
mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.

Amesema Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu,
usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha
kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo ambapo Taifa Stars iliifunga
Morocco mabao 3-1.