SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mwamuzi wa daraja la kwanza (class one), Luteni David Lugenge kilichotokea Septemba 7 mwaka huu kwa ajali ya gari katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Luteni Lugenge ambaye mwishoni mwa wiki alishiriki mitihani ya utimamu wa mwili kwa waamuzi wa Ligi Kuu alikuwa na ndugu yake Christopher Alexander Lunyungu katika gari dogo wakienda mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Handeni, Peter Juma, Luteni Lugenge alikuwa akimsindikiza mwenzake aliyekuwa anakwenda kujitambulisha kwa wakwe zake watarajiwa.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Luteni Lugenge alikuwa ni mmoja wa waamuzi wanaoinukia nchini, hivyo mchango wake ulikuwa bado unahitajika. Hivyo tutamkumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Luteni Lugenge, Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu nchini (FRAT) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.