TFF Kuchunguza Hujuma ya Stars, Yanga Yatakiwa Kuwasilisha Rasimu

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea tuhuma za hujuma kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za kufuzu mashindano ya AFCON.
 
TFF pamoja na kutokuwa na uthibitisho wa tuhuma hizi nzito haliwezi kuzikalia kimya. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania litateua jopo la kuchunguza tuhuma hizi.
 
Wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania (Members of TFF Family) watakaohitajika kuhojiwa na jopo hilo kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za TFF watalazimika kutoa ushirikiano. Atakayeshindwa kutoa ushirikiano atachukuliwa hatua za kimaadili.
 
Pia wadau wa mpira wa miguu ambao sio wanafamilia wa TFF, watakaoitwa na jopo hili wanaombwa watoe ushirikiano kwa nia ya kujenga mpira wetu.

YANGA YATAKIWA KUWASILISHA RASIMU YA KATIBA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Yanga kuwasilisha rasimu ya Katiba waliyoipitisha, kwa kuzingatia kuwa Muhtasari wa kikao cha Mkutano Mkuu wao wa Juni 1 mwaka huu umeainisha baadhi ya marekebisho waliyofanya kwa tulivyowaelekeza.
 
Yanga wanatakiwa kuwasilisha rasimu hiyo kabla ya Oktoba 5 mwaka huu. Ikiwa itakubaliwa na TFF, itapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo ili waweze kufanya uchaguzi wa viongozi wao.