TFDA wazindua maabara ya kimtandao ya ubora wa bidhaa

Baadhi ya bidhaa ambazo TFDA imezifanyia uchunguzi na kubaini zinafaa kutumika kwa walaji.

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imezindua mradi wa kimtandao utakaofanya kazi ya kudhibiti na kulinda ubora wa vifaa anuai kwenye maabara yake ambayo hutumika kuchunguza na kubaini maradhi ya binadamu.

Akizindua mradi huo jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya alisema mradi huo utasaidia kugundua kwa usahihi vifaa na hata kumuelekeza daktari kutoa tiba ki usahihi kwa wagonjwa.

Naibu Waziri pia alipata fursa ya kutembelea maabara ya TFDA ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kufuatilia kwa umakini na kulinda afya za Watanzania hususani katika dawa za vyakula.

Aidha ameongeza kuwa hivi sasa kumekuwa na tatizo kubwa katika upande wa vipodozi jambo ambalo limekuwa likiwasababishia akina mama kupata saratani, hivyo kuitaka taasisi hiyo kuangalia kwa kina namna ya kudhibiti hali hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Dawa na Vipodozi, Mitangu Fimbo amesema kumekuwepo na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo hasa kipindi wanapokwenda kukamata dawa feki.