Na Shomari Binda-Musoma
TIMU ya Soka ya Tessema ya Temeke inashikilia usukani wa Ligi ya Taifa ngazi ya Taifa kituo cha Musoma baada ya hapo jana kuifunga timu ya Nongwa VTC ya Manyara mabao 2-1 na kufikisha pointi 6 na magori 4 ya kufunga baada ya kuitandika timu ya Korogwe United mabao 2-0 katika mchezo wao wa kwanza.
Wachezaji wa timu hiyo wanaoonekana kupania zaidi ligi hiyo baada ya kuonekana kuweka umakini katika michezo yao iliyotangalia huku wachezaji wa timu hiyo wakiahidi kuendeleza wimbi la ushindi ili kuweza kupata nafasi ya kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao.
Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Kassim mohamed Jongo aliliambia Mtanzania bado wanahitaji sapoti na msaada wa karibu kutoka kwa wakazi wa Temeke kwa kuwa utaratibu wa kuwapa msaada wa aina yeyote ulishatangazwa kabla hawajaondoka kutoka Jijijini dar es salam.
Alisema siri ya matokeo mazuri katika michezo yao iliyotangulia ni ushirikiano kutoka kwa viongozi pamoja na wachezaji walioambatana na timu hiyo na kuahidi kundeleza ushirikiano huo ili kufanya vizuri katika michezo inayofuatia ya ligi hiyo ya Taifa ngazi ya Taifa.
Katika msimamo wa ligi hiyo katika mzunguko wa kwanza timu ya Polisi Mara inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 4 kutokana na ushindi wa mbao 2-0 dhidi ya Ashathi united na sare ya bao 1-1 dhidi ya Forest ya Kilimanjaro ikifuatiwa na timu ya Framingo ya Arusha pamoja na Forest ya Kilimanjaro.
Timu ya Ashathi inashika mkia katika kituo hicho cha Musoma baada ya kupoteza michezo yao yote miwili ya mwanzo baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 toka kwa Polisi Mara na kabla ya kupokea kichapo kingine cha mabao 2-1 toka kwa Framingo ya Arusha.
Timu zinazoshiriki ligi hiyo katika kituo cha Musoma ni wenyeji Polisi Mara, Nongwa VTC ya Manyara, Korogwe United ya Tanga, Framingo ya Arusha, Forest ya Kilimanjaro, ashathi ya Ilala, Tessema ya Temeke pamoja na Red Cost ya Kinondoni.