Tenga amkatalia Said Mohamed kujiuzulu

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya TFF, Said Mohamed.

Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa klabu ya Azam alimuandikia Rais Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo akipinga kauli ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Alfred Tibaigana juu ya adhabu zilizotolewa na Kamati ya Ligi kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga.

Rais Tenga amesema alimteua Mohamed katika Kamati hiyo kwa kuzingatia uadilifu wake na uwezo wake katika kuongoza, hivyo amekataa barua hiyo ya kuomba kujiuzulu.

Kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na Mkutano Mkuu wa TFF, Rais Tenga, Oktoba 28 mwaka jana aliunda Kamati ya Ligi ambayo wajumbe wake wanatoka kwenye klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Wallace Karia (Mwenyekiti), Said Mohamed (Makamu Mwenyekiti), Damas Ndumbaro, Steven Mnguto, Geoffrey Nyange, Seif Ahmed, Henry Kabera, ACP Ahmed Msangi, Meja Charles Mbuge na Ahmed Yahya.