Tenga amgomea Aden Rage kujiuzulu

Rais wa TFF, Leodger Tenga

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura kwa vyombo vya habari, alisema Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba alimuandikia Rais Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema ‘kamati hiyo kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira Tanzania zinavyoeleza.’

Amekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa kama Rage amehisi kuwepo udhaifu wa kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea kuwemo kwenye kamati hiyo ili kuisaidia kusimamia sheria na kanuni hizo kama inavyotakiwa badala ya kujiuzulu.

“Kutokana na uzoefu na uwezo ambao Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu, ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu za maendeleo ya mpira wa miguu,” alisema Rais Tenga.

Pia Rais Tenga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo imetoa kwa kamati zote za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala kupendelea upande wowote.

Rais Tenga amesisitiza kuwa kamati hazina budi kuchukua hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa. Amezitaka kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa kufanya hivyo, uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira wa miguu kuongozwa kwa sheria na haki.

Wakati huo huo; Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina kwa ajili ya makamishna (match commissioners), watathmini wa waamuzi (referees assessors) na waamuzi wa daraja la kwanza (class one) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza baadaye mwezi ujao.

Kwa upande wa makamishna na watathmini wa waamuzi, semina itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 29-30 mwaka huu. Washiriki wanatakiwa kujigharamia kwa kila kitu; usafiri, malazi na chakula wawapo kwenye semina.

Semina kwa waamuzi itafanyika katika vituo vya Dar es Salaam na Mwanza kuanzia Agosti 31- Septemba 2 mwaka huu. Pia nao watajigharamia kwa kila tu. Waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni ambao hawakushiriki ile iliyofanyika Juni mwaka huu na wale walioshiriki lakini hawakufaulu mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test).

Waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) hawashiriki kwa vile wao wamekukuwa wakishiriki semina zao zinazoandaliwa na FIFA kila baada ya miezi mitatu.