Temeke UTD, Small Kids kushushana Machi 31

Boniface Wambura Ofisa Habari wa TFF

Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Dar es Salaam jana, Machi 12 mwaka huu imeamua timu za daraja la kwanza za Temeke United na Small Kids zicheze mechi Machi 31 mwaka huu mjini Dodoma ili kupata moja itakayoshuka daraja.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Ligi Daraja la Kwanza timu tatu zitashuka daraja, moja kutoka katika kila kundi. Kwa vile AFC ya Arusha na Manyoni ya Singida kutoka kundi C tayari zimeshashuka, Kamati ya Ligi imeamua Temeke United na Small Kids zilizoshika nafasi ya mwisho katika makundi yao ya A na B zicheze mechi hiyo ili kupata moja itakayokamilisha idadi ya timu tatu za kushuka daraja.

Baada ya kumalizika hatua ya kwanza ya Ligi Daraja la Kwanza, timu tisa zimefanikiwa kucheza hatua ya fainali ya Tisa Bora na nyingine tano za Burkina Faso ya Morogoro, Morani ya Manyara, Polisi ya Iringa, Majimaji ya Songea na Green Warriors (94KJ) zimefanikiwa kubaki Ligi Daraja la Kwanza.

Wakati huo huo; shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea kupokea maombi ya uenyeji wa kituo cha Fainali za Ligi Daraja la Kwanza iliyopangwa kuanza Machi 31 mwaka huu ikishirikisha timu tisa.

Mikoa kadhaa imeshawasilisha maombi ya uenyeji lakini hakuna ambao umekamilisha masharti ya kulipa sh. milioni 25 TFF ikiwa ni gharama za uendeshaji wa fainali hizo.

Baadhi ya mikoa ambayo imeshatuma maombi ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo ni Mbeya, Morogoro, Mwanza, Ruvuma na Tabora. Kamati ya Ligi itatangaza kituo cha fainali hizo baada ya Machi 15 mwaka huu ambayo ni siku ya mwisho kupokea maombi na kutimiza masharti yaliyowekwa.

Timu zilizofuzu kucheza hatua ya fainali kutoka kundi A ni Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga na Transit Camp ya Dar es Salaam. Kundi B ni Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma na Tanzania Prisons ya Mbeya wakati kundi C ni Polisi ya Tabora, Polisi ya Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora.