TEMEKE na Mjini Magharibi zinapambana Septemba 13 mwaka huu katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zimetinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao za robo fainali ya michuano hiyo zilizochezwa Septemba 12 mwaka huu asubuhi kwenye uwanja huo huo. Wakati Temeke imetinga hatua hiyo baada ya kuilaza bao 1-0 Iringa lililofungwa dakika ya 18 na Ramadhan Mohamed, Mjini Magharibi imeing’oa Mtwara kwa ushindi wa bao 1-0.
Robo fainali nyingine zinachezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) jioni kwa Kilimanjaro kuvaana na mabingwa watetezi Morogoro huku Arusha ikioneshana kazi na Ilala.
TFF YATOA ITC KWA WAWILI, MAULID RUKSA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa Watanzania wawili kucheza mpira wa miguu nchini Afrika Kusini.
Wachezaji hao; Robert Kobelo na Mohamed Ibrahim wamepewa hati hizo baada ya kuombewa na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kama wachezaji wa ridhaa ili wajiunge na klabu ya Cacau United ambayo timu yake inacheza Ligi Daraja la Pili katika Wilaya ya Cacau.
Naye mchezaji Said Maulid aliyejiunga na Ashanti United akitokea nchini Angola msimu huu amepata ITC ambayo sasa inamwezesha kuchezea timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoingia mzunguko wake wa tatu keshokutwa (Septemba 14 mwaka huu).