Na Joyce Anae
Tembo wameendelea kuwatesa wananchi wa Rombo mkoani Kilimanjaro,
na kusababisha zaidi ya Kaya 950 kukumbwa na Tatizo la njaa.
Inaelezwa kuwa zaidi ya Tembo 400 huingia kila siku katika maeneo
mbalimbali ya Wilaya hiyo na kufanya uharibifu mkubwa wa Mashamba na
Makazi ya watu hali iliyosababisha Wananchi wengi kukumbwa na Uhaba
mkubwa wa chakula.
Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya
Rombo , Judathadeus Mboya wakati akizungumza na gazeti hili ofisini
kwake kuhusiana na tatizo la uvamizi wa wanyama aina ya tembo katika
wilaya hiyo na jitihada walizochukua ili kukabiliana nalo.
Alisema kumekuwepo na makundi ya Tembo wanaotokea Mbuga za Tsavo na
Amboseli Nchi jirani ya Kenya, ambao wamekuwa wakitembea maeneo
mbalimbali ya wilaya hiyo kwa ajili ya kutafuta Malisho na kusababisha
uharibifu mkubwa wa mazao.
Alisema kutokana na uvamizi huo halmashauri hiyo kwa sasa
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula baada ya mashamba ya
wananchi wengi kuathiliwa vibaya na wanyama hao wanaotokea Nchi
jiarani ya Kenya.
“Wanyama hawa huingia katika wilaya hii kwa ajili ya kutafuta chakula,
na hii ni kutokana na kukosa chakula katika maeneo yao na zaidi ya
hekari 284 zimeharibiwa vibaya na tembo hao ambao waliingia na kula
mazao ambayo yalikuwa hayajafikia kuvunwa hii ni hatari sana na wamekuwa
wakiwasumbua sana Wananchi wa maeneo haya”alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha alisema wanyama hao wamekuwa Tatizo kubwa kwa wananchi wilayani
humo hususani wakulima kutokana na Mazao yao kuharibiwa na kwamba hata
wakati mwingine husababisha Mauaji kwa wananchi ambao mara nyingi
hukutwa shambani .
Alizitaja kata zilizoathiriwa zaidi na wanyama hao kuwa ni kata ya
Holili, Ngoyoni, Mamsera, Mahida, Kirongo Sananga, Tarakea Matamburu,
Tarakea Kitende na kata ya Aleni na kwamba kutokana na jiografia ya
wilaya hiyo Tarafa zote zinapakana na Nchi jirani ya Kenya ambapo
ndiko wanyama hao hutokea.
Kwa miaka mingi sasa kundi la wanyama aina ya tembo wamekuwa
wakivamia maeneo ya wilaya ya Rombo, kwa ajili ya kujitafutia chakula
na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.