JITIHADA kubwa za Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya mifugo na ufugaji wa Tanzania zimepata msukumo mpya kufuatia uamuzi wa kujengwa kwa maabara ya kisasa kabisa ya matumizi ya teknolojia ya vinasaba ya kuboresha mbegu za mimba za ng’ombe inayojulikana kama embryo transfer.
Maabara hiyo ya kisasa itajengwa katika eneo la Ranchi ya Mzeli, mkoani Tanga, na kampuni ya nyumbani ya Overland Livestock Multiplication Unit and Embryo Transfer kwa kutumia teknolojia kutoka nchi ya New Zealand na kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa ya Ranchi (NARCO).
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bwana Feisal Edha akifuatana Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, mtaalam kutoka New Zealand na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya NARCO alimwambia Rais Kikwete mwanzoni mwa wiki hii mjini Dodoma kuwa maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo ambayo itakuwa ya pili ya aina yake katika Afrika Mashariki.
Maabara hiyo inawezesha ng’ombe bora mama bandia (surrogate mother) kupokea mbegu bora kutoka kwa ng’ombe bora mfadhili (donor) na kumlea hadi kutoa ndama wa kisasa kabisa ambao wanazaliwa kwa wingi kulingana na idadi ya surrogate mothers ambao wanaweza kuuzwa kwa wananchi.
Bwana Feisal alimwambia Rais Kikwete kuwa kwa kawaida ng’ombe huzaa ndama 13 katika maisha yake ya wastani wa miaka 13 hadi 16, lakini chini ya teknolojia hiyo, ng’ombe anaweza kutoa mayai kiasi cha 126 kwa mwaka ambayo yanaweza kupandikizwa katika surrogate mothers kwa wakati mmoja baada ya ng’ombe hao kuingizwa katika joto.
Bwana Feisal pia alimwambia Rais Kikwete kuwa teknolojia hiyo inamwezesha mfugaji kuchagua kwa uhakika zaidi anataka kuzalisha ng’ombe wa namna gani – wa maziwa, wa nyama, dume ama jike na kuwa teknolojia hiyo pia ni bora zaidi kuliko ile ya uhamilishaji ambayo ndiyo imeanza kutumika nchini kwa sasa.
Mkurugenzi huyo pia ameongeza kuwa chini ya makubaliano na wabia wake wa New Zealand, watanzania watapelekwa kusomea teknolojia hiyo nchini humo na kuwa New Zealand imekubali kuipa Tanzania teknolojia hiyo moja kwa moja.
Bwana Feisal pia alisema kuwa asilimia ya maboresho yote ya ng’ombe na sekta hiyo duniani inatumia teknolojia hiyo kwa sasa. Rais Kikwete alionyeshwa kufurahishwa kwake na hatua hiyo akisisitiza kuwa amekuwa akielekeza kuhusu umuhimu wa kuleta mageuzi katika ng’ombe na mifugo ya Tanzania kwa miaka yote ya uongozi wake.
“Nimewapenda na kuwaamini sana watu wetu wa mifugo lakini hakuna jambo la maana wamefanya katika muda wote. Nakushukuru Bwana Feisal kwa uamuzi wako huu na nataka kukuhakikishia kuwa kama watu wetu wanakuzungusha, wewe endelea tu na mimi niko tayari kukusaidia,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Nimefurahi kusikia habari hii, sasa nyie endeleeni na mipango yetu ya ujenzi wa maabara, msiingie kwenye urasimu wa hawa watu wetu. Msikubali wawababaishe kwa sababu kama hawa watu wa Wizara ama NARCO hawako tayari kusonga mbele nyie endeleeni tu, wacha wao waendelee to run around in circles.”