TCRA Yazinduwa Kampeni ya Matumizi Mazuri ya Mawasiliano, Yazungumza na Bloggers

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini, Profesa John Nkoma akizungumza katika semina hiyo leo.

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungi akizungumza katika mkutano huo.

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wakifuatilia mada

Baadhi ya washiriki hao wakipiga picha baada ya semina na msanii maarufu nchini, Mrisho Mpoto (Mjomba)

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo.

Na Joachim Mushi, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania leo imezinduwa kampeni ya matumizi mazuri ya mawasiliano, ikiwa na lengo la kuelimisha jamii kutumia mawasiliano vizuri kama ilivyoainishwa katika sheria ya mawasiliano ya kielectroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 kwamba ni kosa kutumia mawasiliano vibaya.

TCRA imeyazungumza hayo leo asubuhi katika semina ya kuwakutanisha wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii Tanzania, ikiwa ni moja ya kampeni za kuelimisha jamii juu ya matumizi ya mawasiliano kwa maendeleo na si vinginevyo.
Akizungumza katika semina hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini, Profesa John Nkoma alisema idadi ya watumiaji wa intaneti imezidi kuongezeka kutoka watumiaji 300,000 (mwaka 2011) hadi kufikia watumiaji milioni 7.6.

Alisema wengi wa watumiaji wa mitandao kama facebook, blog, twitter, BBM na LinkedIn wanafanya hivyo kwa nia ya kujifunza na kujielimisha, hivyo mamlaka inakila sababu ya kupiga vita matumizi mabaya ya mawasiliano ikiwemo mitandao ya kijamii.

“Wengi wa watumiaji wa intaneti matumizi yao ni katika kujifunza na kujielimisha pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, BBM, LinkedIn na Blog anuai zinazotoa habari mbalimbali zikiwemo za kimaendeleo, burudani pamoja na michezo,” alisema Prof. Nkoma.

Alisema katika kampeni hiyo mamlaka inakusudia kuwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia mawasiliano vizuri ili kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania. Aidha aliongeza kuwa katika kampeni hiyo mamlaka imewashirikisha baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii (ikiwemo www.thehabari.com) ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watanzania walio wengi wananufaika na mawsilino. Miongoni mwao mamlaka imezungumza na wamiliki wa blog mbalimbali, wasimamizi wa makundi anuai katika mtandao wa FB na mengineyo.

Alisema lengo la kukutana na makundi hayo ni kuomba ushirikiano ili waweze kushiriki katika kampeni hiyo ya kuhamasisha mashabiki wao kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kunufaisha taifa letu kwa matumizi mazuri.
“Tunawasihi wananchi na watumiaji wa huduma za mawasiliano kuwa wakipokea ujumbe wowote wa kueneza chuki unaoweza kusababisha kuvuruga amani, uchochezi na kuvuruga amani toa taarifa kwa vyombo husika, kasha futa ujumbe huo. Usiueneze kwa wengine kwani utakuwa sehemu ya uhalifu,” alisema Profesa John Nkoma.