TCRA Yazilima Faini Tigo, Airtel, Halotel na Zantel

Baadhi ya logo za makampuni ya Simu Tanzania
MAMLAKA ya Mawasilaino nchini Tanzania (TCRA) imezipiga faini pamoja na kutoa onyo kali kwa makampuni ya simu za mikononi za: Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart), MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo), Airtel Tanzania Limited, Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel), na kampuni ya Zanzibar Telecom Limited (inayojulikana kama Zantel) kwa kile kushindwa kuwalinda wateja wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya TCRA iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk. Ally Y. Simba imefafanua makampuni hayo yameshindwa kutimiza matakwa ya Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Postal ya mwaka 2011 [the Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011] kwa kushindwa kuweza mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano.

TCRA pia imeamuru makampuni hayo kila moja kulipa faini ya Shilingi za Kitanzania Milioni Ishirini na Tano (Shs 25,000,000.00) kwa Mamlaka ya Mawasiliano kabla ya tarehe 29 Januari, 2016; na Endapo Makamuni haya yatashindwa kutimiza amri Na.2 hapo juu, Mamlaka itachukua hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti dhidi ya Kampuni ya Simu husika.

“…Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inapeda kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi kuwa makini na jumbe za kuwataka kutuma fedha bila ya kuwa na uhakika. Inashauriwa kuhakiki ujumbe husika kwa kupiga simu na kuongea na mhusika kabla ya kufanya maamuzi ya kutuma fedha hata kama namba inayotumika unaijua. Vilevile wawe makini wanapopokea jumbe zinazoonesha zinatoka kwa mtu fulani wanayemjua kumbe ni matapeli wanaotumia ulaghai kwa njia hii ya “spoofing”,”.

“Tarehe 16 Oktoba, 2015 Mamlaka iliwakumbusha watoa huduma za simu nchini juu ya wajibu wao kuchukua hatua za kusheria na kitaalamu ili kulinda watumiaji dhidi ya utumaji wa jumbe za kilaghai na kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao kutumika kutuma jumbe za udanganyifu na kulaghai.

“Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mamlaka tarehe 16 Desemba, 2015 Mamlaka ilibaini kuwa kampuni za Benson Informatics Limited (inayojulikana kama Smart), MIC Tanzania Limited (inayojulikana kama Tigo), Airtel Tanzania Limited, Viettel Tanzania Limited (inayojulikana kama Halotel) and Zanzibar Telecom Limited inayojulikana kama Zantel) zimeshindwa, zimepuuzia na zimekataa kufuata maagizo ya Mamlaka kuchukua hatua mara moja kuzuia mitandao yao kutumika kutuma jumbe za kilaghai kinyume na Kanuni Na.8(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011 [the Electronic and Postal Communications (Computer Emergency Response Team) Regulations, 2011]…,” alisema Dk. Ally Y. Simba katika taarifa yake kwa umma.