JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KATIKA KAMATI YA MAUDHUI YA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA DAR ES SALAAM
SHAURI LA UKIUKAJI WA KANUNI ZA UTANGAZAJI
NAMBA 4/2015
DHIDI YA
INDEPENDENT TELEVISION (ITV)
UAMUZI
UAMUZI WA KAMATI YA MAUDHUI KUHUSU LALAMIKO LA UKIUKAJI WA KANUNI ZA UTANGAZAJI, MWAKA 2005
1.0 Utangulizi:
Mnamo tarehe 10/08/2015, kituo cha ITV kilikiuka Kanuni za Huduma ya Utangazaji (Maudhui), 2005 kupitia kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi Punde kilichorushwa hewani kati ya saa 2.30 asubuhi hadi saa 5.30 asubuhi. Kipindi hiki kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutoa taarifa zisizo za kweli na za kichochezi zilizotangaza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya mgombea wa CHADEMA Mheshimiwa Edward Lowassa. Taarifa hiyo ilikuwa na maandishi yaliyosomeka kama ifuatavyo:-
1. “ Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia CHADEMA”.
2. “ Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lakanusha kupiga marufuku maandamano kutokea ofisi za CUF kuchukua fomu Mgombea Urais kupitia CHADEMA.
Katika kuhitimisha taarifa hiyo mtangazaji alisikika akisisitiza kwamba Kamishina Suleiman Kova alisema ni marufuku maandamano ya mgombea wa CHADEMA kupitia UKAWA kwenda kuchukua fomu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mtangazaji alisikika akizungumza maneno yafuatayo:-
“….ni Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova akizungumza na ITV, Radio One pamoja na Capital Radio amesema ya kwamba ni marufuku maandamano ya Mgombea wa CHADEMA kupitia UKAWA Mheshimiwa Edward Lowassa kwenda kuchukua fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi… hizo ndizo taarifa ambazo zimetufikia hivi punde”
2.0 Kanuni zilizokiukwa
Kituo cha ITV kimekiuka Kanuni zifuatazo za Huduma ya Utangazaji (Maudhui) 2005
Na. 5(h), 6(2)(b) na 6(2)(c) ambazo zinazosomeka hivi:-
5 Every licensee shall ensure that the programme and its presentation-
(h) does not incite or perpetuate hatred against or vilify, any
group or persons on the basis of ethnicity, race, gender,
Religion or disability.
6(2) The licensee shall-
(b) report accurately and fairly;
6(2)(c) report news in an objective and balanced manner, without
intentional or negligent departure from the facts, whether by
distortion, exaggeration, misrepresentation or material omission;
Tafsiri ya Kanuni hizi kwa mujibu wa Kamati katika shauri hili ni kama ifuatavyo:-
5. Kila mwenye leseni ya utoaji huduma za utangazaji lazima ahakikishe kuwa vipindi vyake vinazingatia:-
(h) havileti uchochezi wala kujenga chuki kwa mtu au kundi la watu kwa kigezo cha kabila, rangi, jinsia, dini au ulemavu.
6(2) Kila mwenye leseni ni lazima ahakikishe-
(b) anatoa taarifa kwa usahihi na uhakika;
6 (2) (c) anaripoti habari bila upendeleo na kizingatia mizani, bila
kukusudia au kuondoka katika ukweli, ama kwa
kuvuruga au kutoa taarifa zisizo sahihi.
3.0 Ushahidi wa Makosa
3.1 Kuangalia DVD ya kipindi cha “Habari Zilizotufikia Hivi Punde”
Ili kujiridhisha kama maudhui ya kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi Punde na uwasilishaji wake ulikiuka Kanuni za Utangazaji, Kamati na uongozi wa ITV waliangalia sehemu ya kipindi hicho. Maudhui ya kipindi hicho yalionyesha ukiukwaji wa Kanuni za Utangazaji.
4.0 Maelezo ya utetezi
4.1 Maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa ITV
Mkurugenzi wa ITV aliwasilisha utetezi wa maandishi wakukana kuhusu tuhuma zote za ukiukwaji wa Kanuni uliofanywa na kituo chao. Alisema msingi wa habari ulikuwa si wa kichochezi na ilikuwa ombi la Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutoa ufafanuzi wa taarifa za upotoshaji zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Aliendelea kusisitiza kwamba taarifa haikuwa ya kichochezi kutokana na ukweli kwamba watu walikuwa wamekusanyika Buguruni Ofisi ya CUF kwa lengo la kuandamana kumsindikiza Mgombea Urais wa CHADEMA jambo ambalo Kamishna Kova alipiga marufuku. Mkurugenzi pia aliendelea kusema kuwa wakati wakirusha hewani taarifa ya Kamishna Kova walikuwa wanabadilisha maandishi kwenye runinga kulingana na taarifa zilizokuwa zinatolewa na Kamishna Kova.
Aliendelea kusema kwamba pamoja na kutoa taarifa iliyolalamikiwa Kamishna Kova alirudi tena kwenye kituo cha ITV na alitoa taarifa kwa umma kwamba Jeshi la Polisi liliafikiana na viongozi wa vyama hivyo kwamba maandamano yaanzie ofisi za CUF zilizoko Buguruni hadi ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na baadae kuishia Kinondoni katika ofisi za CHADEMA.
4.2 Maelezo ya Mhariri Wa Habari
Mhariri wa Habari wa ITV alitoa utetezi wake kwa kusema kwamba nia ya ITV haikuwa kuleta uchochezi kwa kuwa habari ilikusudia kuondoa upotoshaji wa taarifa kwamba watu waache kwenda mjini kutokana na kuwepo kwa maandamano ya CHADEMA. Alisisitiza kwamba Mtangazaji wa taarifa hiyo hakuwa na nia mbaya wala kusudio la kuchochea uvunjifu wa amani na dhamira yake haikuwa kumfanya Kamishna Kova kuongea anachokitaka yeye kama mwandishi wa habari ila kuondoa hofu kuhusiana na suala zima la maandamano.
4.3 Maelezo
Mwanasheria/Mwakilishi wa ITV alitoa utetezi wake kwa kusema maneno yaliyoandikwa kwenye taarifa hiyo yalikuwa ni vionjo tu vya kumwezesha mtazamaji kuvutiwa na taarifa kisha asikilize na kupata ukweli. Bwana Semvua alitoa mfano wa magazeti yanavyotoa vionjo vya taarifa mbalimbali ambazo humvutia mtu kuisoma habari katika tukio husika.
5.0 Kukiri Kosa
Katika majumuisho yao wawakilishi waliotoa utetezi wa ITV moja baada ya mwingine walikiri kosa na kudai kuwa kituo chao hakina kawaida ya kuitwa mbele ya Kamati kwa makosa na wao kama binadamu hawakuwa na dhamira ya kusababisha vurugu nchini kwa kuwa binadamu hukosea.
Mhariri wa Habari ITV alisisitiza kwamba haikuwa nia yao kuleta uchochezi na wala mtangazaji wa taarifa hiyo hakuwa na nia mbaya. Mhariri wa habari alizungumza maneno yafuatayo:-
“Mwenyekiti tunakushukuru, tunaomba mtuelewe kwamba muktadha wa tukio lote hili haukuwa na nia mbaya, kwa maana ya kwamba nia mbaya haikukusudiwa…hakukuwepo na kusudio, hakukuepo na nia mbaya na ovu yoyote kupeleka lile tukio liwe na tafsiri ya watu kwa jinsi walivyo lipokea…”
Mwanasheria/Mwakilishi alisema lengo halikuwa kufanya kosa hilo kwa makusudi na naomba mtuchukulie hivyo tulifanya kosa kwa bahati mbaya, makosa yapo kwa binadamu na tafsiri ya kimtazamo ni kawaida kukosea na ilikuwa ni bahati mbaya watajirekebisha. Alisema maneno yafuatayo:-
“Makosa yapo ya kila mwanadamu, tulifanya hivyo tudhani tumefanya vizuri na ndio maana tulidhani tutapongezwa, lakini mtizamo wa wenzetu kwa kweli imeonekana na tulivyosikia…si kweli kwamba tunaonewa asilimia mia moja.. ukiangalia ITV na Redio One siyo vituo vinanyoletwa letwa huku mara nyingi na ikitokea mtuchukulie kwamba imetokea kwa bahati mbaya kama wanadamu na sisi tutajirekebisha kwa haya mliyotuadvise…..”
Aidha Mkurugenzi wa Radio One alikiri kwamba lengo lilikuwa zuri na kusudio lilikuwa kuondoa uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii. Bwana Deo Rweyunga alisema yafuatayo:-
“…wito wenu ni wa nia ya kutaka kujirekebisha ili tuende vizuri pamoja, mmetuandikia tumejieleza, tumekaa pamoja na tumezungunza pamoja, lengo lilikuwa ni zuri tujaribu kuondoa uvumi ambao ulikuwa tayari kwenye mitandao….tukiri katika hili ambalo limeonekana kidogo ni tofauti, tutachukua hatua kama inavyofahamika vyombo vyetu tumekuwa tunajitahidi sana na tumeteleza kidogo tunaomba mtuwie radhi kwa hilo”
Mkurugenzi Mtendaji alisema Breaking News ya Tanzania inavyoendeshwa ni vigumu kuipata, tunaomba radhi kwa hilo lililotokea haikuwa dhamira yetu, tutahakikisha tunaedelea na dhamira yetu ya kutoa matangazo kwa ubora. Kubwa lilituleta ni mwanzo na mwisho wa taarifa yenyewe na waliomba radhi na kuhakikisha watafanya kazi kwa umakini. Alisema maneno yafuatayo:-
“…pamoja na hayo kubwa ambalo limetuleta ambalo tumeliona ni mwanzo na mwisho…na marekebisho ambayo tuliona tukarekebishe tukiwa hewani ni kwamba tunaomba radhi kwa hilo kwa sababu sisi tulikuwa tunaongea kwa upande wetu jinsi tunavyofanya kazi…..tunaomba radhi kwamba limetokea hivyo liliyotokea na hivyo lilivyopokelewa huko nje…na haijawa dhamira yetu wala nia yetu ya kuvuruga hii nchi…”
6.0 Tathmini ya Kamati
Kamati iliridhika kwamba, kituo cha ITV katika kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi Punde kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutoa taarifa zisizo za kweli na za kichochezi zilizotangaza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya mgombea wa CHADEMA Mheshimiwa Edward Lowassa.
Kamati iliona upungufu katika maneno yaliyoandikwa kwenye runinga (subtitling) wakati Kamisha Kova akihojiwa. Katika utangulizi wa Habari Zilizotufikia Hivi Punde mtangazaji alisikika akisema kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia CHADEMA. Mtangazaji alisikika akimhoji Kamishna Kova kutoa ufafanuzi kuhusu kupiga marufuku maandamano. Kamishna Kova alisikika akisema alichukua nafasi hiyo kuwapigia ITV na Radio One kuondoa uvumi uliokuwa umeenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa Polisi wamepiga marufuku maandamano ya Kumsindikiza Mheshimiwa Lowassa kuchukua fomu za kugombea Urais katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kamishna Kova alisema Polisi ilikuwa imepanga kuwapa ulinzi wasindikizaji wa Mgombea Urais Mheshimiwa Lowassa kupitia CHADEMA kutoka ofisi za CHADEMA Kinondoni mpaka ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama Jeshi la Polisi lilivyotoa ulinzi kwa wasindikizaji wa mgombea Urais Kupitia Chama Cha Mapinduzi DKt John Magufuli. Kamisna Kova alisisitiza kuwa haikuwa jambo jema kwa maandamano kutokea kila sehemu ya jiji kwa vile kungeweza kuleta uvunjifu wa amani na kuathiri shughuli zingine za wananchi. Kamisna Kova alisisitiza kuwa:-
“………ukiwazuia watu kwa kwenda tu kuchukua fomu hapo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na njia tunayoisema ambayo tunaitambua ni hiyo ambayo mimekueleza na ninachukua fursa hii kukanusha kabisa maelezo hayo siyo ya kwetu na hata jinsi ilivyoandikwa hili tangazo siyo model yetu na namna yetu ya kuandika taarifa…kwahiyo tunaomba pia watu wasipotoshe watu na masuala ya Kipolisi ni nyeti mno na mtu asijaribu kutengeneza taarifa za kupotosha watu kupitia Kiongozi wowote wa Jeshi la Polisi….”
Mwandishi katika kuhitimisha Habari Zilizotufikia Hivi Punde alirudia na kusisitiza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia CHADEMA. Hii ni kinyume na utetezi uliotolewa na uongozi wa ITV na Radio One kwamba walikuwa na nia ya kusaidia kutoa ufafanuzi juu ya uvumi ulioneea kwenye Mitandao kuwa Polisi walipiga marufuku maandamano.
7.0 Uamuzi wa Kamati
Kamati iliridhika kuwa kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi Punde kilichorushwa hewani na kituo cha ITV tarehe 10/08/2015 kilikiuka Kanuni za Utangazaji.
Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi kutoka viongozi wa ITV na Radio One, Kamati ya Maudhui inaamua yafuatayo:-
1.1 ITV inapewa onyo kali; na,
1.2 ITV inatakiwa kukanusha na kuomba radhi katika taarifa yake ya Habari ya saa mbili usiku na asubuhi kwa siku mbili mfululizo baada ya kusomwa kwa uamuzi huu.
Endapo ITV itakiuka tena Kanuni za Utangazaji, hatua kali zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Uamuzi huu umetolewa na kusomwa Dar es Salaam siku hii ya tarehe13 Mwezi wa Agosti Mwaka 2015.
Haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu iko wazi ndani ya siku 30 tangu uamuzi unapotolewa.
Uamuzi umetolewa na:
Mhandisi Margaret T. Munyagi
Mwenyekiti
Na:
WAJUMBE WA KAMATI YA MAUDHUI
1. Bwana Walter Bgoya
2. Bwana Joseph Method Mapunda
3. Bwana Abdul Ramadhani Ngarawa
13 AUGUST 2015