Moshi,
WAFANYABIASHARA wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), mkoani Kilimanjaro wameishauri Serikali kuhakikisha inawawajibisha walimu wanaokiuka maadili ya kazi yao na kujenga uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi, hali inayochangia kwa kasi kushuka kwa kiwango cha taaluma eneo hilo.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Kilimanjaro, Patrick Boisafi wakati akizungumza na wandishi wa habari waliotaka maoni ya taasisi hiyo juu ya kuibuka mchezo wa walimu kujenga mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.
Boisafi alisema kiwango cha kuporomoka kwa maadili kwa walimu nchini kwa sasa kinazidi kukua, hali ambayo inasababishwa na sababu anuai ikiwemo changamoto za ufinyu wa mishahara ya walimu na upungufu wa walimu hapa.
Alisema moja ya vitendo vya uvunjifu wa maadili ambavyo vimekuwa vikifanywa na walimu ni kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao bila kujali hali ambayo imekuwa ikisababisha kutoheshimiana shuleni na hivyo kuchangia kiwango cha taaluma kuzidi kuporomoka.
Alisema ufike wakati sasa serikali iwawajibishe walimu watakaobainika kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi na si kuhamishwa vituo vyua kazi ilihali ya kwamba wamebainika kufanya makosa.
Alisema walimu wengi wamekuwa wakihamishwa vituo vya kazi pindi wanapobainika kufanya makosa hali ambayo hupelekea kosa hilo kuendelea hivyo ni vema sheria ikachukua mkondo wake pindi mwalimu anapobainika kukiuka maadili na kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi na kama sheria hizo zinaonekana hazitoshelezi ni vema pia zikaongezwa makali ili kuondoa kabisa tatizo hilo.
“Kumekuwepo na walimu wengi ambao wamekuwa wakikiuka maadili ya kazi zao huku wengine wakiwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao, hivi mwalimu akishakuwa na mahusiano hayo na mwanafunzi anaweza kumuonya tena kitu au kumuelekeza wakasikilizana au ndo kudharauliana, kimsingi ni kwamba sheria zipo na nadhani zinafahamika zichukuliwe kukomesha tatizo”alisema Boisafi.
Alisema pamoja na kuwajibishwa kwa walimu wenye mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi pia walimu wanaokwenda shule na vimini au milegoze waangaliwe kwani nao wamekuwa wakichangia kushuka kwa nidhamu mashuleni.
Aidha aliwataka pia walimu kuipenda kazi yao na kuhakikisha wanazingatia vema maadili ya kazi licha ya kuwepo mapungufu na changamoto mbalimbali katika kazi yao ikiwemo upungufu wa walimu na ucheleweshwaji wa mishahara.
“Walimu wamekuwa na malalamiko mengi na moja ya malalamiko yao ni ucheleweshwaji wa mishahara na upungufu wa walimu lakini walimu wasifanye hayo kuwakigezo cha kukiuka maadili yao kwa kuona kwamba kuna upungufu hivyo hawawezi kufukuzwa kazi, ni vema wakazingatia vema maadli ya kazi ili kutimiza malengo ya Serikali,” alisema.