Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesema kuenea kwa bidhaa duni na bandia nchini husababishwa na hali ya kupanda kwa bei za bidhaa halisi na zenye ubora unaotakiwa ikilinganishwa na bei za bidhaa duni na bandia.
Taarifa hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo (TBS) , Charles Ekelege wakati akifungua semina kwa maofisa wa Jeshi la Polisi kuhusu umuhimu wa jeshi hilo kupambana na wimbi la bidhaa bandia Tanzania.
Mkurugezi huyo amesema TBS imeweka mipango na mikakati kwa ajili ya kuhamasisha jamii juu ya ubora wa bidhaa ikiwemo uwekaji wa alama za TBS kwenye bidhaa zilizothibitishwa ubora na shirika, ukaguzi wa mara kwa mara wa kushtukiza sokoni kwa ajili ya kudhibiti uhalifu huo.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa kwa kuzingatia majukumu ya Jeshi la Polisi, TBS inaliomba jeshi hilo kufanya kazi kwa kushirikiana zaidi na ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi, doria na misako maalumu dhidi ya waagizaji, waigizaji na wasambazaji wa bidhaa duni kama inavyofanyika kwa wahalifu wengine.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Sheria TBS, Baptistery Bitaho amesema katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, shirika limeanzisha mfumo mpya wa kukagua bidhaa za aina zote katika nchi zinapotoka, bidhaa ambayo haina ubora unaotakiwa haitaruhusiwa kusafirishwa na kuingia nchini.
Amebainisha sheria mpya inampa mamlaka Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko kuteua wakaguzi ambao wanakuwa na mamlaka ya kuingia sehemu yoyote ya uzalishaji wa bidhaa na kukagua ubora wa bidhaa hizo. Waziri pia anayomamlaka ya kuondoa bidhaa hafifu sokoni na kutoa tangazo kwa umma kuhusiana na uhafifu wa bidhaa hiyo hatari na madhara yake.
Ametoa wito kwa kila raia kuhakikisha kuwa anatumia bidhaa zilizohakikishwa na kuthibitishwa na shirika la viwango Tanzania, yaani bidhaa zilizo na alama ya ubora ya TBS. Sambamba na hilo amesema kila raia anatakiwa kuwa makini dhidi ya wanaozalisha au kuingiza bidhaa zisizo na ubora Tanzania
Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi nchini, Emmanuel Kandihabi amesema kuwa changamoto kubwa inayolikabili jeshi la polisi nchini ni baadhi ya wananchi na wafanyabiashara kukosa uaminifu, uzalendo, maadili na utaifa jambo linalochangia kuzidi kuingiza, kutengeneza,kununua na kuuza bidhaa bandia kwa lengo la kukimbilia bei ndogo au kujitajirisha kwa haraka
Amesema Jeshi la polisi litaendelea kushirikiana na mamlaka zinazohusiana na udhibiti wa bidhaa bandia katika kuratibu na kusimamia mikakati ya oparesheni za pamoja kwa kuboresha na kuimarisha ushirikishwaji , mawasiliano na umakini ili kufikia mafanikio.