Tatizo la umeme sasa ni janga la taifa-Mnyika


John Mnyika Mbunge wa Ubungo na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kambi ya upinzani.

TATIZO sugu la mgawo wa umeme ambalo sasa limekomaa na kuwa janga la taifa limetokana na ufisadi na udhaifu wa kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini kuanzia awamu ya pili, likaongezeka katika awamu ya tatu na kukomaa katika awamu ya tatu ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufisadi na udhaifu huo wa kiutendaji unajidhihirisha zaidi katika maamuzi mbalimbali yaliyofanyika wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi (hususani 1990 mpaka 1995), Rais Benjamin Mkapa (hususani 1996 mpaka 2004) na Rais Jakaya Kikwete ( hususani 2006 mpaka 2011) kwenye matendo na mikataba mbalimbali mathalani kashfa ya IPTL, hasara ya mchakato wa ubinafsishaji wa TANESCO, uzembe wa Net Group Solution, ufisadi wa Kiwira, kashfa ya Alstorm Power Rentals, sakata la Songas/Pan African Energy, ufisadi wa Richmond, madhara ya Dowans (ambayo sasa mitambo yake iko chini ya Symbions) ambapo mkazo haukuwekwa katika mipango ya muda mrefu ya kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme nchini ambayo imetajwa bajana katika nyaraka mbalimbali za mipango ya kiserikali.

Hivyo ufumbuzi wa tatizo hili katika hatua ya sasa ambapo taifa limefikia unahitaji uongozi na uwajibikaji wa ngazi za juu zaidi katika mihimili ya dola ya serikali, bunge na mahakama katika kuchukua hatua zinazostahili kwa kushirikisha wadau wengine hususani sekta binafsi badala ya kutegemea Wizara ya Nishati na Madini.

Katika muktadha huo nawapongeza Umoja wa Wafanyabiashara wa Makampuni Makubwa 55 nchini (CEOrt) kwa tamko lao kuhusu mgawo wa umeme na naitaka serikali hususani Rais Kikwete kuzingatia na kuchukua hatua za haraka kuhusu madai yaliyotolewa na watendaji wakuu wa makampuni hayo kupitia kwa mwenyekiti wao.

Rais Kikwete kwa nafasi yake ya kuongoza mhimili mmoja wa dola anapaswa kuitisha kikao cha baraza la mawaziri na kufanya maamuzi mazito yenye kuhusisha kutangaza mgawo wa umeme kuwa ni janga la taifa na kuunganisha wadau wote katika kuchukua hatua za dharura; ili kuweka uzito wa kiutendaji katika kauli ya kisiasa iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.

Kwa upande mwingine Spika wa Bunge kwa wajibu wake wa kuongoza mhimili mwingine wa dola anapaswa kutumia kanuni ya 53 (2) au 55 (1) au 114 (17) kuwezesha kuwepo kwa mjadala bungeni kwa ajili ya kupitisha maazimio ya dharura ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme kutokana na kauli ya serikali ama Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini kama sehemu ya wajibu wa kikatiba wa Bunge wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Izingatiwe kwamba katika tamko lao watendaji hao wameeleza athari za kiuchumi za mgawo wa umeme unaondelea kwenye kushuka kwa mapato ya serikali na pia kupungua kwa ajira; madhara ambayo yamewahi kuelezwa pia na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) mwezi Februari mwaka 2011.

Aidha katika tamko lao kama lilivyonukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 2 Julai 2011 wameeleza kwamba serikali imekuwa ikitoa kauli za kisiasa na kutaja miradi bila hatua za haraka na mkakati bayana wa kiutekelezaji hususani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012. Pia, katika tamko lao wameeleza tatizo la umeme kuwa ni janga la taifa na kutaka serikali iitishe mjadala wa kitaifa utakaohusisha pia sekta ili kupata majibu ya kitaalamu na kushirikiana katika utekelezaji.

Tamko hilo limesadifu kauli ambazo nimezitoa kuhusu mgawo wa umeme hususani tarehe 15 Februari 2011, tarehe 2 Aprili 2011, tarehe 22 Mei 2011 na tarehe 25 Juni 2011 na kuweka bayana hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na serikali kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu mbalimbali.

Hata hivyo, mwelekeo wa matatizo ya mgawo wa umeme umevuka uwezo wa Wizara ya Nishati na Madini na kuwa tatizo la kitaifa ambalo linahitaji uwajibikaji wa pamoja katika serikali ndio maana tarehe 30 Juni 2011 nilitaka kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kutumika kupata majibu. Baada ya kanuni kupindishwa kumlinda Waziri Mkuu Pinda kutoa kauli ya pamoja kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni kwa niaba ya Rais nilitoa mwito kwa Waziri Mkuu Pinda kutumia majumuisho ya mjadala wa bajeti ya wizara yake kutoa majibu.

Lakini Waziri Mkuu Pinda hakutumia nafasi hiyo kueleza hatua za dharura ambazo zinachukuliwa na serikali kukabiliana na mgawo wa umeme pamoja na kufahamu kwamba yeye mwenyewe katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 aliahidi kwamba mitambo ya umeme ya MW 100 Ubungo na MW 60 Mwanza ingenunuliwa kwa wakati; suala ambalo kama angelisimamia ipasavyo lingeweza kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kupunguza kwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa.

Kutokana na Waziri Mkuu kutokutoa kauli kuhusu dharura ya mgawo wa umeme katika hotuba yake ya bajeti tarehe 23 Juni 2011 na wakati wa majumuisho ya hotuba hiyo tarehe 1 Julai 2011 ilinibidi nishikilie mshahara wake kwa mujibu wa kanuni 101(3) kupata maelezo wakati bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Tarehe 1 Julai 2011 nililieleza bunge kuwa mgawo wa sasa umesababishwa na udhaifu wa kiutendaji wa kutokufanya maandalizi kwa wakati ikiwemo kuchelewa kufanya manunuzi kwa ajili ya mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya IPTL, kuchelewa kutekeleza miradi wa MW 100 Ubungo, MW 60 Mwanza na MW 260 kupitia mitambo ya dharura na kutaka ufafanuzi kutoka kwa Waziri Mkuu. Hata hivyo, ufafanuzi haukutolewa na Waziri Mkuu badala yake maelezo yalitolewa na Waziri wa Nishati na Madini ambayo hayakujitokesheleza.

Kadhalika lipo tatizo na upungufu wa nishati ya kuendeshea mitambo ya umeme ikiwemo upungufu wa mafuta mazito na gesi asilia hali ambayo isipochukuliwa hatua za dharura itasababisha mgawo wa umeme kuendelea hata baada ya mitambo ya dharura kuletwa nchini. Hivyo, mapitio ya haraka ya mikataba ya uwekezaji wa gesi pamoja na ujenzi wa Bomba la Gesi ambao haukuzingatiwa kikamilifu katika bajeti ya serikali 2011/2012 inapaswa kufanyika. Maamuzi hayo magumu yanapaswa kuambatana na hatua za kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa nishati na pia katika uingizaji wa vifaa vyenye kusaidia kupunguza makali ya mgawo wa umeme. Hivyo, ni muhimu Rais Kikwete akatimiza wajibu wake wa kikatiba kwa kuingilia kati tatizo la mgawo wa umeme kwa kurejea pia maelekezo yake ambayo aliyatoa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 15 Februari 2011 na ahadi alizozitoa kwa taifa katika hotuba yake ya tarehe 1 Aprili 2011. Hatua hizo zitaepusha matamko yanayoendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari badala yake uwajibikaji wa pamoja wa dharura utafanyika kupitia baraza la mawaziri, bunge na mikutano na wadau muhimu kukabiliana na janga la taifa la mgawo wa umeme.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

3 Julai 2011; Bungeni-Dodoma