TATIZO LA MAJITAKA HOSTELI ZA MABIBO KUPATIWA UFUMBUZI

Na Veronica Kazimoto–MAELEZO

5/07/2011

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umekiri kuwapo kwa tatizo la maji taka yanayotoka katika Hosteli za Mabibo kuelekea Mto Kisiwani ulioko Ubungo Kisiwani jijini Dar es Salaam, hali inayosababisha kero kubwa kwa wananchi wanaoishi karibu na hosteli hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala, Prof. Yunus Mgaya kupitia Idara ya Habari MAELEZO, uongozi huo unatarajia kuwa na kikao cha kujadili namna ya kuondoa tatizo hilo ambalo linaleta adha na usumbufu mkubwa kwa wakazi wa Ubungo hasa wale wanaolizunguka eneo la hosteli hizo.

“Tunajua tatizo hili limekuwa kero kwa sasabu majitaka yanayotiririka kuingia mto Kisiwani yanasababisha harufu mbaya kwa wananchi wa Ubungo na sasa hivi tunaitisha kikao kitakachojadili namna ya kuondoa tatizo hili,” amesema Prof. Mgaya.

Prof. Mgaya amefafanua kuwa kwa kipindi hiki watafanya kila mbinu ya kuimarisha mfumo uliopo pamoja na kutengeneza jenereta kwa ajili ya kusukuma majitaka hayo kutoka Hosteli za Mabibo kwenda Mabwawa saba (Mabibo mwisho).

Naye Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) Jackson Midala amesema, tatizo hilo la majitaka eneo la Ubungo linachangiwa pia na wananchi wenyewe; kwani hutumia kigezo cha Hosteli ya Mabibo kufungulia maji machafu yanayotoka katika vyoo vyao kuelekea mto Kisiwani.

“Baadhi ya wananchi waishio karibu na maeneo ya Hosteli za Mabibo wanachangia kwa kiasi kikubwa kutiririsha majitaka kutoka katika nyumba zao kuelekea mto Ziwani kwa kusingizia kuwa yanatoka kwenye hosteli hizo,” amefafanua midala.

Aidha Midala amekitaja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa chanzo kingine cha tatizo hilo kwa kuwa Hosteli za Mabibo zinaongozwa na chuo hicho hivyo ni wajibu wake kuhakikisha kuwa mfumo wa majitaka katika eneo hilo unatunzwa vizuri.

Hata hivyo Midala kupitia ofisi yake ameahidi kushirikiana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kupitia vyombo vya habari kuwa, wakazi waishio kuzunguka Hosteli ya Mabibo wanapata adha kubwa kutokana na kutiririka kwa majitaka kutokana na kufurika kwa mifereji eneo hilo.