JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
TARATIBU ZINAZOFUATWA KATIKA UVUNAJI WA MAZAO YA MISITU KWENYE SHAMBA LA SAO HILL
Wizara ya Maliasili na Utalii inatoa ufafanuzi kuhusu taratibu zinazofuatwa katika uvunaji wa mazao ya misitu katika shamba la miti la Saohill.
Baadhi ya magazeti ya tarehe 19 Mei 2011 yaliandika kuhusu uvunaji wa mazao ya misitu katika Shamba la Miti la Saohill lililoko Mufindi mkoani Iringa. Habari hiyo inahusu tuhuma kwamba mawaziri wawili na mbunge mmoja wamepewa vitalu vya kuvuna kwa ufisadi katika Msitu wa Saohill.
Habari hiyo inayohusu ufisadi siyo ya kweli maana wananchi hao ni kati ya wale walioomba kuvuna miti kwa kufuata taratibu zote zinazoruhusu uvunaji katika mashamba ya miti ya Serikali.
Ufafanuzi unatolewa kuwa shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu hufanyika kwa kuongozwa na nyaraka mbalimbali za Serikali. Kwa sasa uvunaji unafanywa kwa kufuata ‘Mwongozo wa Uvunaji Endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu’ wa mwaka 2007, ambao unaonyesha taratibu muhimu za kufuatwa katika shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu.
Mwongozo huo unatokana na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, pamoja na Matangazo ya Serikali (Government Notices) Namba 69 na 70 ya mwaka 2006.
Sheria ya Misitu haimzuii mwananchi yeyote kuvuna mazao ya misitu kutoka kwenye misitu ya asili au ya kupandwa mradi awe amefuata taratibu zilizopo katika nyaraka husika.
Shughuli za ugawaji wa mazao ya kuvuna katika kila shamba la Serikali hufanywa na Kamati ya Ugawaji Mazao ya Misitu ya sehemu husika.
Kamati hiyo ni ya Wajumbe watano:-
(i) Mkurugenzi Msaidizi (Matumizi ya Misitu) au mwakilishi – Mwenyekiti
(ii) Afisa Misitu Mkoa au Mshauri wa Maliasili Mkoa – Mjumbe
(iii) Meneja wa Shamba – Katibu
(iv) Msaidizi wa Meneja wa Shamba – Mjumbe
(v) Bwana miti wa eneo ambalo miti itavunwa – Mjumbe.
Utaratibu uliopo ni kuwa mwananchi anayehitaji mazao kutoka katika misitu ya mbao laini hupeleka maombi yake kwa Meneja wa shamba linalohusika, nakala Wizarani, kuanzia Januari 1 hadi tarehe 30 Aprili kila mwaka. Maombi hayo yanatakiwa yapokelewe mapema maana Kamati ya Ugawaji hukaa mwezi Juni kila mwaka.
Mhe. Cyril Chami, Mhe.William Lukuvi na Mhe George Simbachawene ambao walitajwa katika taarifa hiyo ya magazeti ni kati ya wananchi waliopeleka maombi yao kwa meneja wa shamba la Sao Hill ya kutaka kuvuna miti kwa kufuata taratibu zilizopo. Kamati ilipokaa kujadili maombi ya watu wote walioomba, wao ni kati ya wale waliopewa kibali cha kuvuna.
Sababu mojawapo iliyowafanya wapate miti ya kuvuna ni kutokana na maombi yao ambayo yalionyesha kuwa walikuwa hawavuni kwa matumizi yao binafsi, bali ni kwa matumizi ya shughuli za maendeleo ya wananchi katika majimbo yao.
Wizara inasisitiza kuwa mwananchi yeyote anayo haki ya kuvuna mazao ya misitu mradi afuate taratibu zilizopo kisheria, na kuwa atakachouziwa ni miti, wala siyo kumilikishwa kitalu.
George Matiko
MSEMAJI WA WIZARA
Tarehe 20 Mei 2011