Tanzanite ya Tanzania Yawafuata Young She-Polopolo

Tanzanite mazoezini na kocha wao.

Tanzanite mazoezini na kocha wao.


TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania wenye umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) wanatarajiwa kuondoka kesho jumatano asubuhi kwa Rwanda Air kuelekea nchini Zambia kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Young She-Polopolo.

Tanzanite inayowania kufuzu kwa Fainali za Kombe Duniwa mwaka 2016 nchini Papua New Guinea, itacheza mchezo huo wa marudano siku ya jumamosi tarehe 25 Julai, jijini Lusaka. Katika mchezo wa awali uliofanyika takribani wiki mbili zilizopita, Tanzanite ilipoteza mchezo wake nyumbani baada ya kufungwa kwa mabao 4 – 0, hivyo kuhitaji kushinda zaidi ya mabao 5 – 0 ili kuweza kusonga katika hatua inayofuata.

Msafara wa Tanzanite utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo utajumuisha makocha Rogasian Kaijage (kocha mkuu), Edna Lema (kocha msaidizi), Peter Manyika (kocha wa makipa), Christina Luambano (Daktari), Mwanahamis Abdallah (mtunza vifaa) na Meneja Furaha Francis.

Wachezaji watakaosafiri ni Stumai Abdallah, Shelder Boniface, Donisia Minja, Najiat Abbas, Neema Kiniga, Happyness Mwaipaja, Jane Lucas, Anastazia Katunzi, Anna Mwaisura, Janet Pangamwene, Gelwa Rugomba, Blandina Ambros, Amina Ramadhan, Asha Shaban, Maimuna Hamis, Zuwena Hamis, Amisa Athuman na Wema Richard.

PL KUANZA SEPTEMBA 12
Ligi Kuu ya Tanzania (PL) itaanza Sept 12 badala ya Agosti 22 ili kumpa Charles Mkwasa fursa ya kuendelea na program yake kuelekea mechi ya Taifa Stars vs Nigeria itakayochezwa Sept 5. Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) itakayozikutanisha Azam FC dhidi ya Yanga SC sasa itachezwa Agosti 22 badala ya Agosti 15.

Ratiba ya Ligi Kuu iliyokuwa imeandaliwa, sasa inafanyiwa marekebisho kwa ajili ya tarehe mpya ya kuanza, ambapo pamoja na mambo mengine mechi sasa zitachezwa wikiendi na katikati ya wiki na wikiendi ya Oct 25 hakutakuwa na mechi kupisha Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge. Klabu za Ligi Kuu zimeandikiwa barua kujulishwa tarehe mpya ya kuanza Ligi, na dirisha la usajili linabaki kama lilivyo.

Wamiliki wa viwanja vyenye upungufu wmeandikiwa barua kutakiwa kurekebisha upungufu katika muda maalumu, vinginevyo havitaruhusiwa kutumika kwa ajili ya PL na FDL. Timu ya Madini ya Arusha imeruhusiwa kutumia Uwanja wa Nyerere uliopo Mbulu mkoani Manyara kwa mechi za SDL kwa masharti upungufu uliopo kwenye uwanja huo urekebishwe kwanza.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)