TANZANIA imesema kuwa itaunga mkono ombi na jitihada za Jiji la Tokyo
katika Japan kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020.
Msimamo huo wa Tanzania umetangazwa Alhamisi, Mei 30, 2013 na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu
wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe.
Katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu wa Japan,
Abe aliiomba Tanzania kuiunga mkono katika jitihada zake
kadhaa za kimataifa ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kuandaa
Michezo ya Olimpiki mwaka 2020.
“Nina maombi mawili kwako Mheshimiwa Rais…moja ni kwamba Jiji la Tokyo ni moja ya miji ambayo inawania kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020. Tunaomba kuungwa mkono na Tanzania na tunaomba usaidie tuweze kuungwa mkono na Afrika,” Mheshimiwa Abe amemwambia Rais Kikwete.
Baada ya Abe kutoa ombi hilo, Rais Kikwete amesema:
“Tutaiunga mkono nchi ya Japan na Jiji la Tokyo kuweza kuandaa Michezo
ya Olimpiki mwaka 2020. Aidha, nataka kukuhakikishia kuwa tutatumia
mahusiano yetu katika Afrika kuwezesha kuungwa mkono kwa ombi hilo la
Japan.”
Jiji la Tokyo ni miongoni mwa miji mitatu duniani ambayo imevuka hatua
ya kwanza kutoka mji iliyoomba (applicant cities) na kuwa mji
inayoweza kuandaa Michezo ya Olimpiki (candidate cities). Miji mingine
miwili ni Madrid (Hispania) na Istambul (Uturuki).
Kabla ya hatua hiyo, miji mitano ikiwamo Tokyo, Madrid na Istambul
pamoja na Baku (Azerbaijan) na Doha (Qatar) ilikuwa imeomba kuandaa
Michezo hiyo kabla ya idadi yao kupungua Mei 25, 2012.
Uteuzi wa mwisho wa Mji ambao utandaa Michezo hiyo utatangazwa
kufuatia kikao cha 125 cha Kamati ya Utendaji ya Kamati ya Olimpiki
Duniani (IOC) kilichopangwa kufanyika Septemba 7, 2013 mjini Buenos
Aires, Argentina.
Tokyo mara ya mwisho iliandaa Michezo ya Olimpiki mwaka 1964.