Tanzania Yaunga Mkono Malengo Endelevu ya Maendeleo Duniani

Tanzania Yaunga Mkono Malengo Endelevu ya Maendeleo Duniani
TANZANIA imeunga mkono rasmi Malengo Endelevu ya Maendeleo (Sustainable Development Goals – SDG’s), ikisisitiza kuwa, kwa hakika, malengo hayo ni silaha ya kutosha ya kufuta umasikini duniani katika sura zake zote ifikapo mwaka 2030.

Tanzania pia imesema kuwa endapo dunia itafanikiwa kutekeleza SDG’s katika miaka 15 ijayo kama ilivyopangwa ni dhahiri kuwa ifikapo mwaka 2030 dunia itakuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa ajili ya “watoto wetu na watoto wa watoto wetu.”

Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa Septemba 26, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalojadili kwa nia ya kupitisha SDG’s chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke Rusmussen.

Rais Kikwete ameliambia Baraza Kuu hilo kuwa ni vyema vile vile nchi zilizoendelea kuelewa fika kuwa pamoja na kwamba nchi zinazoendelea zitalenga kutimiza wajibu wake wa msingi wa kuzalisha fedha za ndani kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizo, bado juhudi pekee za nchi zinazoendelea hazitatosha kuhakikisha utekelezaji kamili wa agenda hiyo ya maendeleo endelevu inayojulikana rasmi kama, “Transforming our World: The 2030 Agenda for Sustainable Development.”

“Juhudi za nchi zilizoendelea zitaongeza nguvu katika juhudi zetu wenyewe ambazo nazo zina ukomo. Ni ushirikiano huu kati ya walioendelea na sisi tunaoendelea ambao utatuhakikishia utelekezaji kamili wa malengo mapya ya maendeleo endelevu. Tafadhalini endeleeni kutushika mkono. Hili ndilo jambo la maana zaidi, bora zaidi na la ukweli zaidi kwa ajili ya faida yetu sote.”

Rais Kikwete amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ikiwa ni mwendelezo wa shughuli zake mjini New York, Marekani, ambako anahudhuria mikutano mbali mbali ya Baraza Kuu la UN mwaka huu ambayo kimsingi yote inalenga katika kujenga msingi mzuri wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu mapya katika mambo mbali mbali.

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia – Millennium Development Goals (MDG’s) ambayo utekelezaji wake wa miaka 15 umefikia mwisho mwaka huu. Wakati MDG’s ulikuwa na malengo manane, SDG’s una malengo 17 na shahaba za kukamilishwa 169.
Rais Kikwete pia amegusia baadhi ya changamoto ambazo zilikuwa ni kikwazo kwa nchi nyingi zinazoendelea duniani kilichozifanya nchi huzo kushindwa kufikia malengo yote ama baadhi yake ikiwamo changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutosha na kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa MDG’s.

“Ni muhimu kulitaja jambo hilo, kama jambo muhimu na jambo kuu, kwa sababu ilikuwa ni hali ya ukosefu wa uhakika wa upatikanaji wa raslimali fedha ambao ulikuwa kikwazo kikubwa kuliko vyote katika utekelezaji wa MDG’s,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Ni jambo linalonipa faraja, hata hivyo, kuwa katika mpango wa malengo mapya ya maendeleo endelevu, jambo hilo limefafanuliwa na kupewa umuhimu pekee. Upatikanaji wa raslimali fedha wenyewe ni lengo linalojitegemea, lengo nambari 17, ambalo linaelezea jinsi gani ya utekelezaji wa kila mojawapo ya malengo hayo.”