RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameshtushwa na kusononeshwa sana na taarifa za kifo cha Rais wa Jamhuri ya Zambia, Michael Chilufya Sata ambacho kimetokea jana, Jumanne, Oktoba 28, 2014 kwenye Hospitali ya King Edward VII, London, Uingereza, ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa miaka 77.
Katika salamu ambazo amempelekea Makamu wa Rais wa Zambia, Mheshimiwa Dk. Guy Scott kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi, habari za kusikitisha za kifo cha Mheshimiwa Michael Chilufya Sata, Rais wa Jamhuri ya Zambia.
Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe Mheshimiwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu, na kupitia kwako familia ya wafiwa na ndugu wa Hayati Rais Sata pamoja na Serikali na ndugu zetu wananchi wote wa Zambia kufuatia msiba huu wa ghafla.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hayati Sata atakumbukwa daima kama mmoja wa viongozi wa mfano wa kuigwa katika Afrika. Katika kipindi chake kifupi cha uongozi wa juu wa Zambia, alifanikiwa kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Zambia. Atakumbukwa pia kwa imani yake isiyoyumba ya kupigania uhuru, haki na usawa, sifa ambazo zilimfanya kiongozi mpendwa ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Zambia.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Hivyo, huyu ni kiongozi ambaye siyo tu atakumbwa na wananchi wa Zambia lakini atakumbukwa na sisi sote wenzake na watoto wote wa Afrika.”
“Katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na huzuni, tunaungana nanyi kuomboleza na kumwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira wana familia ya wafiwa, jamaa na ndugu zetu wote wa Zambia ili waweze kuhimili machungu ya kipindi hiki cha msiba mkubwa. Aidha, tuko pamoja nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema roho ya Marehemu Michael Chilufya Sata.”