Na Joachim Mushi
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars imetinga hatua ya Nusu Fainali baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Malawi bao 1-0, katika mchezo mkali na wa kuvutia uliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kilimanjaro Stars ambayo ilicheza kwa kujihami mchezo huo, mpaka inakwenda mapumziko, ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na mchezaji wake Nurdin Bakari dakika ya 36 kwa shuti kali akiwa umbali wa sentimita 30. Kipindi cha kwanza cha mchezo kila timu ilifanya mashambulizi kadhaa na mara nyingine kukosa nafasi nyingi za wazi.
Mchezaji, Hussen Javu nusura aiandikie Stars bao katika dakika ya 10 baada ya kupata pande maridadi kutoka kwa Mrisho Ngassa lakini alijikuta akipoteza nafasi hiyo. Hadi dakika 90 za mchezo huo zikikatika Kilimanjaro ilikuwa mbele kwa goli moja na Malawi ikiambulia patupu.
Kwa ushindi huo sasa Kilimanjaro Stars ya Tanzania itacheza na timu ya Taifa ya Uganda ambayo iliifunga Zimbabwe 1-0, Katika mchezo wa kwanza zilipokutana (Zimbabwe na Uganda) kumtafuta kinara. zimbabwe imeaga mashindano haya baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, goli lililopatikana dakika ya 14 likifungwa na Hamis Kiiza kwa kichwa akimalizia pasi ya Sula Matovu. Mpaka sasa timu za wageni zilizoalikwa zimeyaaga mashindano hayo na kuacha timu za Ukanda wa Afrika Mashariki.