Na Rungwe Jr.
California, USA
Mwisho wa Juma lililopita nilikuwa Santa Barbara, California, moja kati ya miji mizuri sio tu Marekani, bali duniani kwa ujumla. Baada ya uchovu wa kuzunguka hapa na pale, nikaamua kuingia kwenye Mgahawa maarufu wa ‘Starbuck’ ili kupata kikombe cha kahawa!(Sio kikombe cha Babu!) Nilipoingia tu ndani ya Mgahawa nilikaribishwa na picha hii ya mnyama Tembo na juu yake chapisho kubwa la jina la nchi yetu ‘Tanzania’. Baada ya kujisachi haraka haraka, nikagundua kuwa nilikuwa nimeacha Kamera yangu ndani ya gari, hivyo basi, nikarudi chapchap kwenye gari, ili nichukue Kamera na kupata ukumbusho wa picha hii. Baadhi yenu mnaweza mkahoji umuhimu wa habari hii, na kufikiri pengine hamna lolote la ajabu.
Ndugu zangu, dev.kisakuzi.com inaipa umuhimu habari hii kutokana na ukweli kwamba Tanzania haijulikani sana nje ya mipaka ya Tanzania, haswa haswa Ulaya na Marekani. Hivyo basi, kutuwia vigumu kufanya biashara katika maeneo haya, ukizingatia ule usemi usemao “Biashara ni matangazo”. Ukitembea Ulaya na Marekani, sio ajabu sana kuona mabango ya ndugu zetu Wakenya katika maeneo ya Migahawa au sehemu nyingine za biashara, hivyo basi nchi yao kufahamika zaidi ya yetu. Kwa mantiki hii sio ajabu pia kusikia Wakenya wanadai kuwa Mlima Kilimanjaro upo kwao! Wewe haujawahi kusikia madai haya?
Niliamua kufanya mahojiano kidogo na Meneja wa Mgahawa huu wa Starbucks kuhusiana na picha hii, akanieleza kuwa waliiweka ukutani tokea mwezi wa nane mwaka jana. Waliiweka kutokana na sababu za kuitangaza kahawa ya Tanzania, ambayo ilikuwa inapatikana hapo Mgahawani. Mpaka naondoka mitamboni, jitihada za kufahamu kwanini Kahawa ya Tanzania haipatikani tena Mgahawani hapo hazikuweza kuzaa matunda.Baadhi wa wateja wa Starbucks wakiwa wanabofya Internet na huku wakipata kahawa taratibu.