Tanzania Yasonga Afrika Mapambano Dhidi ya Ukatili kwa Watoto

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka (kushoto) akiwasilisha kubainisha vyombo vya habari vilivyo msaada katika kuripoti vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka (kushoto) akiwasilisha kubainisha vyombo vya habari vilivyo msaada katika kuripoti vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia.

TUNAPOELEKEA kuuanza mwaka 2015, tumeshuhudia vyombo vya habari nchini vikiwa mstari wa mbele katika kubaini na kutangaza matukio ya ukatili na utelekezaji wa watoto unaofanywa na akina dada, wazazi ama ndugu wa karibu sana na watoto husika. Kuongezeka huko kwa taarifa za ukatili dhidi ya watoto ni matokeo ya juhudi mahsusi zinazotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na asasi nyingi za kiraia ikiwemo TAMWA.

Wakati taarifa za matukio hayo zikiongezeka kadri muda unavyozidi zipo pia taarifa za baadhi ya waliowahi kutelekezwa wakiwa watoto na baadaye kulelewa na wafadhiri ama vituo vya malezi ya watoto, wakijitokeza hadharani kupitia vyombo hivyo hivyo vya habari wakitafuta ndugu ama jamaa zao kwa lengo la kutaka kuunganishwa nao tena.

Kwa jinsi hali ilivyo inaonyesha kuwa kwa kiasi fulani kumekuwa na mwamko wa kijamii wa utoaji wa taarifa unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaochukizwa na uwepo, ama kuendelea kwa ukatili dhidi ya watoto katika jamii ya watanzania. Baadhi ya taasisi za umma na zisizo za kiserikali (AZISE) pia zimeongeza juhudi katika kutoa elimu kwa jamii na kuhakikisha kuwa kila tukio linalohusu ukatili dhidi ya watoto ama yatima linatolewa taarifa katika vyombo vya kisheria.

Hata hivyo bado hali ya ukatili huo ni kubwa mno kulinganisha na taarifa zinazofika kwenye mkondo wa sheria. Agosti 9, 2011 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilizidua matokeo ya utafiti ulioendeshwa na Chuo kikuu cha Sayansi na Tiba cha Muhimbili kwa niaba ya Serikali chini ya ufadhiri wa Shirika la Watoto Duniani la UNICEF na CDC ya Marekani. Utafiti huo uliendeshwa kubaini viwango vya ukatili dhidi ya watoto kwa Tanzania bara na visiwani.

Baadhi ya wanahabari na wadau wa asasi zinazopinga ukatili wakiwa katika warsha ya hamasha kwa vyombo vya habari kuripoti ukatili iliyoratibiwa na Tamwa.

Baadhi ya wanahabari na wadau wa asasi zinazopinga ukatili wakiwa katika warsha ya hamasha kwa vyombo vya habari kuripoti ukatili iliyoratibiwa na Tamwa.

Katika ya matokeo ya utafiti ilijitokeza kuwa angalau watoto wa kiume watatu kati ya kumi kwa Tanzania bara na binti mmoja kati ya saba kwa Zanzibar walikuwa wameshahusishwa na ukatili uliosababishwa na watu wazima ama ndugu wa karibu kabla ya kufokisha miaka 18. Pia asilimia 25 ya watoto walioshiriki kwenye utafiti waliwahi kujeruhiwa kihisia na kwa sababu hiyo kiakili na watu wenye umri mkubwa zaidi yao.

Juhudi hizo ni mwendelezo wa kazi nzuri iliyoanza muongo uliopita kwa Serikali kutunga Sera na Sheria ya Ulinzi wa mtoto na baadaye kutengeneza mpango maalum wa kwanza uliojulikana kwa lugha ya kiingereza “The National Costed Plan of Action (NCPA-I) ambao utekelezaji wake ulianza mwaka 2007 na kumalizika mwaka 2011. Tathmini ya mpango huo ilipelekea kuandaliwa kwa mpango wa pili (NCPA II) ambao kwa sasa upo katika hatua za utekelezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya tathmini ya NCPA I hadi Septemba 2012 zaidi ya watoto 269,000 waliokuwa wakiishi katika mazingira hatarishi waliwezeshwa kuondokana na hali hiyo huku zaidi ya watoto 50,000 wakiwezeshwa kiuchumi na asasi za kiraia na za kidini.

Inakadiriwa kuwa asilimia hamsini(10%) ya watoto Tanzania wanaishi katika mazingira magumu na kukosa huduma muhimu kiuchumi, kijamii na kisaikolojia. Mpango wa awamu ya pili ulizinduliwa Februari mwaka jana na Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (MB). Mpango huo unategemewa kutekelezwa hadi mwaka 2017.

Kufuatia utafiti huo ambao ni sehemu ya mchakato wa uboreshaji wa haki na ulinzi wa mtoto Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mashirika ya UNICEF, Save the Children na Plan International kwa ufadhiri wa Jumuiya ya Ulaya (European Union) imejipanga kushughulika na tatizo la ukatili dhidi ya mtoto kwa mikoa ya Pwani, Shinyanga na Zanzibar.

Semina ya wanahabari na wadau wa asasi mbalimbali zinazopambana na ukatili wa kijinsia ikiendelea hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Semina ya wanahabari na wadau wa asasi mbalimbali zinazopambana na ukatili wa kijinsia ikiendelea hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Mradi huo ulizinduliwa mwezi Januari mwaka huu na unategemewa kuendeleza juhudi zilizoanzishwa na Serikali kuhusiana na ukatili dhidi ya Mtoto. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa taarifa za matukio ya ukatili kwa watoto hazifiki kwenye vyombo vya kisheria ama taasisi zinazoweza kuwasaidia wasifanyiwe ukatili huo.

Kwa upande taasisi zilizo mstari wa mbele katika ulinzi wa haki za Mtoto Serikalini, Jeshi la polisi nchini limekuwa mpokeaji mkuu wa taarifa ama kesi zinazohusu utelekezaji wa wototo na ukatili dhidi yao. Tumeshuhudia katika jeshi hilo pia likianzishwa dawati la jinsia lenye kushughulika na kesi pamoja na matukio ya unyanyasaji kijinsia kwa waathirika. Kwa kiasi fulani ukatili wa kijinsia kwa namna moja kuna mahusiano na vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto.

Serikali ya Tanzania imekuwa ya kwanza barani Afrika kufanya utafiti juu ya ukatili dhidi ya watoto wa kike na wa kiume. Matokeo na taarifa ya utafiti huo vilikamilika mwaka 2011. (Joseph Kayinga ni mwandishi wa habari mwandamizi aliyejikita katika taaluma ya huduma za Ustawi wa Jamii. Hivi karibuni aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa kwanza wa shirikisho la vyama vya wataalamu hao barani Afrika na Katibu Mwenezi wa chama cha wataalamu wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini-TASWO. Anapatikana kupitia +255 713-640 072).