Na Magreth Kinabo – Maelezo
SERIKALI imesema haijawafukuza wakimbizi nchini huku akitoa ufafanuzi kuwa zoezi linaloendelea hivi sasa ni linahusiana kuwabaini na kuwarejesha kwao wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiishi hapa nchini kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga kufuatia vyombo vya habari vya nje ya nchi kutangaza kuwa Serikali ya Tanzania imewarudisha kwao kwa nguvu wakimbizi 25,000 kutoka nchi ya Burundi katika kipindi cha muda wa mwezi mmoja uliopita.
“Hakuna mkimbizi yeyote aliyerudishwa Burundi, kwa hiari wala kwa nguvu katika kipindi kilichotajwa. Kipindi cha mwisho cha kuwarejesha wakimbizi kwa hiari kilikuwa mwaka 2012, ambapo hadi Desemba mwaka huo wakimbizi 34,000 kutoka Burundi waliokuwa katika kambi ya Mtabila, iliyoko Kigoma walirejeshwa makwao kwa hiari kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi (UNHCR) na Serikali ya Burundi,” alisema Nantanga.
Alisema Serikali Tanzania bado inaendelea kuwapa hifadhi wakimbizi kuendelea kuishi kwenye kambi na makazi yaliyopo hapa nchini, ambapo jumla ya wakimbizi 264,000 wanapata hifadhi.
“Hadi leo wapo wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wapatao 64,172 kwenye kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu, wakimbizi 175,473 kutoka Burundi wapo kwenye makazi ya wakimbizi ya Mishamo na Katumba wilayani, mkoa wa Katavi na Bulyankulu mkoani Tabora.
Pia wamo wakimbizi 2,128 kutoka Somalia kwenye makazi ya Chogo wilayani Handeni, Tanga, wakimbizi 22,227 kwenye wilaya ya Kasulu na Kigoma vijijini.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba vyombo zoezi la kuwarudisha wahamiaji hao lilianza Agosti mwaka huu. Lakini kabla ya hapo walipewa muda wa wiki mbili kurejea kwao kwa hiari ama kupata vibali halali vya kuwawezesha kuendelea kuishi hapa nchini.
“Hadi Septemba 4, mwaka huu zaidi wahamiaji haramu 27,000 walikuwa wamerejea kwao kwa hiari. Wahamiaji hawa haramu walikuwa katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Rukwa.
Baada ya muda waliopewa wa kuondoka au kujisajili kihalali kuisha, Serikali sasa imeaanza operesheni ya kuwabaini wahamiaji hao waliokaidi wito wa kuwataka kuondoka kwa hiari,” alisema Nantanga.
Nantanga aliongeza kuwa operesheni hiyo inafanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha kuwa wanaokamatwa na kurejeshwa kwao ni wahamiaji haramu kweli na sio raia au wageni wenye hati halali za kuishi hapa nchini.
Aidha alisema Serikali inatoa wito kwa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kushirikiana na Serikali kutoa taarifa sahihi kwa kuwasiliana na mamlaka husika pale wanapopelekewa taarifa zenye utata.