Na Eleuteri Mangi – MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imetiliana saini mkataba wa msaada wa zaidi ya Shilingi Bilioni 134 sawa na Euro milioni 59.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kusaidia sekta ya kilimo na usafirishaji nchini. Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Servacius Likwelile kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa EU nchini Filberto Sebregond leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Dk. Likwelile alisema kuwa sehemu ya msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 82.4 ambazo ni sawa na Euro milioni 36.5 utatumika kuendeleza sekta ya kilimo na kukuza uchumi nchini kwa kupitia kituo maalum cha uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini Tanzania (SAGCOT) na kuboresha miundombinu ya barabara za ukanda huo.
Vilevile Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu iliyobaki ya msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 51.9 ambazo ni sawa na Euro milioni 23 itatumika kuimarisha biashara na ushirikiano katika jumuiya kwa kuanzisha kituo cha pamoja cha ukaguzi mipakani (OSIS).
“Vituo hivyo vya ukaguzi mipakani vitakuwa na manufaa si kwa Tanzania tu, bali hata katika nchi mbalimbali zinazopakana na Tanzania,” alisema Dk. Likwelile.
Alifafanua kuwa msaada uliosainiwa unamanufaa kwa wananchi kwa kuboresha miundombinu vijijini na kusambaza umeme vitu ambavyo vitasaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Naye Balozi wa EU nchini Filberto Sebregond alisema kuwa anaamini msaada huo utasaidia juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuongeza nafasi za ajira, kupungua kwa bei za bidhaa mbalimbali na kuendelea kukuza uchumi nchini. Balozi huyo alisema kuwa EU inaamini kuwa ushirikiano wake na Tanzania utaendelea kuimarika kwa kuhimiza maendeleo kwa pande zote mbili na amani ya watu wake.
Hafla hiyo ya kusaini mkataba ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha, Nishati na Madini, Uchukuzi na Ujenzi, EAC, DFID, SAGCOT, wajumbe kutoka EU, Shirika la maendeleo ya Ufundi kutoka Ubelgiji na washirika wa maendeleo.