RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa Tanzania imekubali kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa ndani ya chama tawala cha Sudan Kusini cha Sudanese People’s Liberation Movement (SPLM), mgogoro ambao umesababisha kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa usuluhishi huo utakuwa wa kichama na Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kitaongoza usuluhishi huo katika mazungumzo yatakayofanyika Arusha na kuwa jitihada hizo za Tanzania hazitaingilia mazungumzo ya kujaribu kusimamisha mapigano nchini humo yanayoendelea huko Addis Ababa, Ethiopia.
Rais Kikwete amesema kuwa ulikuwa uongozi wa SPLM na hasa Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Salva Kiir ambao wameiomba Tanzania kusaidia jitihada za kisiasa za kupatanisha pande ambazo zinavutana na kutofautiana ndani ya SPLM wakiamini kuwa mapatano ndani ya chama yatafanikisha kumaliza mgogoro wa kisiasa katika Serikali ya nchi hiyo ambayo imegawanyika na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Rais Kikwete ametangaza jitihada hizo za upatanishi za Tanzania wakati alipohutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi na kupitia kwao Taifa kwenye Sherehe ya Kuzima Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Kilele cha Wiki ya Vijana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Rais Kikwete amewaambia wananchi kuwa Tanzania imekubali kuwasaidia ndugu zao wa Sudan Kusini kwa nia ya kutimiza wajibu wake wa kimataifa na kwa kuongozwa na kaulimbiu ya Oktoba Mwaka 1959 ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliitoa wakati nchi ya Tanganyika bado ikidai uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza.
Rais Kikwete ameikariri kaulimbiu hiyo maarufu: “Sisi Watu wa Tanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambako hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”
Rais Kikwete amesema kuwa Mwenge wa Uhuru unabeba falsafa kubwa ndani yake kuhusu “nchi yetu na uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge, wenye dhiki na wasiokuwa na amani. Dhamira hii ya Mwalimu na nchi yetu ilitimizwa Desemba 9, 1961, siku Tanganyika ilipopata Uhuru ambako Bendera ya Taifa huru la Tanganyika na Mwenge wa Uhuru vilipandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro na Mwenge kuwashwa.”
“Toka wakati huo mpaka sasa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na majimbo, wilaya na mikoa ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania. Kwa kuzingatia ujumbe uliobebwa na Mwenge wa Uhuru, nchi yetu na sisi Watanzania tumejitolea kwa hali na mali kusaidia ndugu zetu Barani Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa kutoka kwenye makucha ya wakoloni na wabaguzi wa rangi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni fahari kwetu kwamba wananchi wa Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini nao wako huru na tumetoa mchango wetu. Ni jambo la faraja kubwa kwamba nchi yetu imeweza kupatia hifadhi ndugu zetu wa nchi jirani na hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya kukosekana kwa amani ama kukimbia mateso ya uongozi wa kidikteta. Ndugu zetu wa Kongo, Burundi, Rwanda, Kenya na Comoro wanaujua ukweli huo. Na, kwa Uganda tuliwasaidia kuling’oa Dikteta Idd Amin na Comoro tulisaidia kuunganisha nchi yao tena.”