Tanzania imezidi kufanya vibaya katika mizania ya rushwa katika nchi tano za ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya kupanda kutoka nafasi ya nne iliyokuwa ikiishikilia mwaka jana hadi ya tatu mwaka huu.
Burundi inashika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Uganda, ya tatu Kenya, huku Rwanda ikiwa ya mwisho katika mizania ya rushwa Afrika Mashariki.
Matokeo hayo yamo kwenye ripoti ya Kipimo cha Hali ya Rushwa Afrika Mashariki (EABI) 2011, iliyozinduliwa jijini Dar es Saalam jana.
Utafiti huo ulifanywa na taasisi zinazojishughulisha na utafiti katika nchi za ukanda huo, ikiwamo Fordia, Transparency International ya Uganda na Rwanda, Association Burundaise des consommateur ya Burundi, kati ya Februari na Mei, mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Fordia, Bubelwa Kaiza, alisema katika hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo jana kuwa utafiti huo ulizingatia sampuli ya hali ya rushwa katika taasisi zinazotoa huduma kwa umma.
Alisema katika utafiti huo, Jeshi la Polisi limetajwa kuongoza katika mizania ya rushwa kati ya taasisi zinazotoa huduma kwa umma, likifuatiwa na Mahakama na Uhamiaji.
Kaiza alisema Jeshi la Magereza limeshuka katika mizania ya rushwa katika nchi hizo, kutoka nafasi ya sita liliyokuwa likiishikilia mwaka jana hadi ya 18 mwaka huu.
Hata hivyo, alisema Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hazimo kwenye taasisi zinazotoa huduma kwa umma zilizopimwa katika utafiti huo.
Alisema rushwa Tanzania imeongezeka kutoka asilimia 28.6 mwaka jana hadi asilimia 31.6 mwaka huu, wakati rushwa Burundi, ambayo inashika nafasi ya kwanza, imeongezeka kutoka asilimia 36.7 mwaka jana hadi asilimia 37.9 mwaka huu.
Kaiza alisema rushwa Uganda imeongezeka kutoka asilimia 33.0 mwaka jana hadi asilimia 33.9 mwaka huu.
Hata hivyo, alisema rushwa Kenya imepungua kutoka asilimia 31.9 mwaka jana hadi asilimia 28.8 mwaka huu, wakati rushwa Rwanda, ambayo ni ya mwisho katika mizania ya rushwa, imepungua kutoka asilimia 6.6 mwaka jana hadi asilimia 5.1 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka jana Burundi ilishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Uganda. Kenya ilishika nafasi ya tatu, Tanzania ya nne na Rwanda ya tano.
Kaiza alisema katika utafiti huo, jumla ya watu 12,924 walihojiwa. Kati yao, Burundi watu 1,401, Kenya (2,943), Rwanda (2,325), Tanzania (3,522) na Uganda (2,733).
“Hali ya rushwa Afrika Mashariki si nzuri…Rwanda ni nzuri,” alisema Kaiza.
Alisema kwa upande wa Jeshi la Polisi, hakuna mabadiliko makubwa katika rushwa na kwamba, katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) rushwa bado ni kubwa.
Kaiza alisema licha ya kushuka kidogo katika mizania ya rushwa kutoka asilimia 84 mwaka jana hadi asilimia 82.7 mwaka huu, Jeshi la Polisi Tanzania bado liko juu kwa rushwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti, Udhibiti na Takwimu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Yohana Madadi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Edward Hoseah, katika hafla hiyo jana, alisema ripoti hiyo ni nzuri, hivyo watatitumia kuangalia namna ya kumaliza tatizo hilo katika taasisi zilizoguswa.
Mrakibu wa Polisi, James Kasusura, aliyemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, katika hafla hiyo, alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Fordia, lakini akasema jeshi hilo halivumilii vitendo vya rushwa.
Alisema kwa kuzingatia hilo, mwaka 2009 IGP alianzisha makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalum cha kufuatilia, kuangalia na kupambana na rushwa ndani ya jeshi hilo.