Makocha 20 wa Tanzania wanaofanya kozi ya Leseni A kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), wamemaliza kozi hiyo hatua ya kwanza na kusema, “Tumenolewa na sasa tumeiva vya kutosha,” amesema mmoja wa wanafunzi hao, Wilfred Kidao leo saa Julai 30, 2016 wakati Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Kidao amesema japo kozi hiyo ilikuwa hatua ya kwanza ‘Module 1’ kwa sasa wameiva kiasi kwamba watakapomaliza Novemba, mwaka huu wana uhakika wa kupeleka vyeti vyao sehemu yoyote duniani kuomba kazi na kushinda kwa kuwa wameiva vilivyo. Wakufunzi wa kozi hiyo walitokea CAF, Sunday Kayuni na Salum Madadi ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF.
Baada ya kusikiliza kauli hiyo ya Kidao, Rais wa TFF Jamal Malinzi moja kwa moja akawasisitiza makocha hao kufanya kazi kwa juhudi na kuwaeleza kuwa hatua waliyofikia ni kubwa kwa kuwa baadhi ya makocha kutoka nje hawana vyeti na kukosa sifa ya kufundisha timu kubwa ikiwamo timu za mataifa ngazi mbalimbali.
Rais Malinzi alitaka makocha hao kuangazia mpira wa miguu kwa wavulana wengi wakiwa wanatokea katika mashindano yanayodhaminiwa na Kampuni ya simu ya Airtel pamoja na soko la wasichana ambalo kwa sasa linashika chati kila kona ya dunia.
Naye, Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia alimpongeza Rais Malinzi kwa namna anavyoratibu na kuzikubali kozi mbalimbali za waamuzi na makocha. “Kwa muda mrefu au tuseme kwa miaka mingi hakujafanyika kozi nyingi kama kipindi cha uongozi wako ukisaidiana na mimi pamoja na kamati nzima ya utendaji pamoja na sekretarieti.”
“Fanyeni utafiti ninyi makocha. Utaona kuwa sehemu kubwa nchi za Afrika zimefanikiwa kwa kutumia makocha wazawa. Leo ninyi ni makocha wa ngazi ya juu kabisa hivyo mna uwezo wa kufanya vema na kusaidia timu zetu na timu za taifa,” alisisitiza Karia.