*Yashukuru ujenzi hospitali ya magonjwa ya moyo
TANZANIA imeiomba Jamhuri ya Watu wa China kuongeza idadi ya madaktari wake inaowatuma Tanzania kama msaada kutoa huduma ya tiba kama njia ya kuzidi kusaidia kukabiliana na upungufu wa madaktari nchini.
Aidha, Tanzania imeishukuru China kwa kujenga hospitali kubwa inayoweza kulaza wagonjwa 100 kwa wakati mmoja wa magonjwa ya moyo na yenye uwezo wa kuwafanyia wagonjwa wa moyo operesheni. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametoa ombi hilo na shukurani Oktoba 25, 2014 wakati alipokutana na kuzungumza na Mheshimiwa Jiang Yikang, Katibu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) cha Jimbo la Shandong, jimbo ambalo tokea mwaka 1968 limekuwa linatuma madaktari kutoka jimbo hilo kuja nchini kusaidia kutoa huduma ya tiba.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara rasmi ya Kiserikali katika China alisimama kwa siku nzima katika mji mkuu wa Jimbo la Shandong wa Jinan akiwa njiani kutoka Beijing kwenda Jimbo la Shenzhen ambako atafanya. Rais Kikwete na ujumbe wake ambaye amesafiri kwa treni iendayo kasi kutoka Beijing, amewasili kwenye Kituo cha Treni cha Jinan Magharibi kiasi cha saa 5:53 na kupokelewa na viongozi wa Serikali na wa CPC wa Jimbo hilo, siyo mbali na nchi jirani ya Korea kusini.
Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Yikang: “Tunalishukuru sana Jimbo la Shandong ambalo kwa miaka 46 tokea mwaka 1968 limekuwa linatuma madaktari wake kuja Tanzania kutoa huduma ya tiba kwa msaada. Tumepokea makundi 23 ya madaktari zaidi ya 1,000 ambao huja kila baada ya miaka miwili. Tunalishukuru sana Jimbo hilo kwa msaada huu mkubwa.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Lakini bado tunazidi kuwaomba muendelee kutusaidia. Tunahitaji madaktari wengi zaidi kwa sababu uwiano kati ya daktari na wagonjwa nchini kwetu bado ni mkubwa. Katika mazungumzo yangu na Rais Xi Jinping jana nilitoa ombi hili, lakini nalitoa tena hapa kwa sababu madaktari wanatoka Jimbo hili.”
Rais Kikwete pia amelishukuru Jimbo hilo kwa msaada uliowezesha kujengwa kwa Hospitali ya Moyo kwenye Hospitali Kuu ya Taifa ya Muhimbili, Dar Es Salaam. “Hospitali hii ya kisasa kabisa sasa imeanza kufanya kazi. Imeiweka nchi yetu kwenye ngazi tofauti kabisa. Tunawashukuru sana kwa kuendelea kuuunga mkono.”
Jimbo la Shandong ni la tatu kwa utajiri na uchumi imara katika China ambalo pato lake mwaka jana lilikuwa ni dola za Marekani bilioni 882.9 kiasi kikubwa kuliko nchi nyingi za Afrika zikiwekwa kwa pamoja. Thamani ya biashara kati ya Jimbo hilo na Tanzania kwa maka jana ilikuwa dola za Marekani milioni 470. Baadaye jioni, Rais Kikwete alikutana na baadhi ya madakati waliopata kufanya kazi katika Tanzania na akawashukuru kwa mchango wao katika maendeleo ya huduma ya tiba nchini.
Amewaambia madaktari hao kwenye Hospitali Kuu ya Jimbo la Shandong: “Nimeomba niwaone ili niwashukuru sana kwa kuokoa maisha ya watu wetu. Mnashikilia nafasi ya pekee katika mioyo ya Watanzania. Kama mnavyojua fika, madaktari wa Shandong wamekuwa wanatusaidia katika Tanzania tokea 1968 na mpaka sasa kiasi cha madaktari 1223 wametusaidia. Kuna wakati lilikuja hapa kundi kubwa la madaktari 84 kwa wakati mmoja. Nyie mnajua Kiswahili – Nasema asanteni sana.”
Hospitali hiyo ni moja ya hospitali za Jimbo hilo ambazo zimekuwa zinapeleka madaktari wake Tanzania tokea mwaka 1968. Mwaka huo, hospitali hiyo iliweka katika kundi la madaktari waliokwenda Tanzania madaktari wake wanne. Katika miaka yote 46, Hospitali hiyo imepeleka Tanzania madaktari 70 na kwa sababu ya kazi hiyo nzuri Mei mwaka 2004, Rais Benjamin William Mkapa aliitembelea Hospitali hiyo, akakutana na kuwashukuru madaktari waliokuwa wametoa ujuzi wao kuokoa maisha ya Watanzania. Hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 1897, ina historia ya miaka 117 ya kutoa huduma za tiba.
Wakati huo huo, Rais Kikwete ametembelea Kampuni ya Kompyuta ya Inspur iliyoko mjini Jinan na baada ya kutembelea Kampuni hiyo ameondoka mjini Jinan kwenda mji wa Shenzhen ambako atafanya ziara ya siku mbili.