TANZANIA imeiomba Japan kusaidia upatikanaji wa walimu wa hisabati na sayansi na namna ya kufundisha walimu wa masomo hayo nchini kama namna haraka ya kukabiliana na uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo nchini.
Aidha, Tanzania imeiomba Japan kusaidia katika uchapishaji wa vitabu vya sayansi na hisabati ili kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa Tanzania anakuwa na nakala yake ya vitabu vya masomo hayo kama namna ya kuongeza ubora wa elimu.
Tanzania imetoa maombi hayo kwa Japan, Juni 3, 2013, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Ushirikiano na Misaada ya Kimataifa la Japan (JICA) Dk. Akihiko Tanaka kwenye Hoteli ya Intercontinental Yokohama.
Rais Kikwete amekuwa katika Japan kwa ziara ya siku saba ya kikazi akihudhuria Mkutano wa Tano wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD V) ambao umefungwa asubuhi ya leo. Rais Kikwete anaondoka Japan kesho asubuhi kwenda Singapore kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili kabla ya kurejea nyumbani.
Rais amemwambia Dk. Tanaka kuwa moja ya changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu ambayo imepanuka sana nchini katika miaka saba iliyopita ni ukosefu wa walimu wa hisabati na sayansi, masomo ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi.
“Kuna mambo mawili ambayo nataka kuomba msaada wa JICA. Tuna tatizo kubwa la ukosefu wa walimu wa hisabati na sayansi. Tuna uhaba wa kiasi cha walimu 26,000 wa hisabati na sayansi lakini vyuo vyetu vyote vinaweza kutoa wahitimu 2,200 tu kwa mwaka. Hii ina maana ili kuziba pengo hilo tutahitaji kiasi cha miaka 12 ambao ni muda mrefu sana. Hivyo, tunaomba kuona namna JICA na Japan mnaweza kutusaidia katika hili,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mbali na ukosefu wa walimu wa hisabati na sayansi ambalo sasa limekuwa jambo la dharura kabisa, napenda pia kuiomba Japan kupitia JICA kuweza kuisaidia nchi yetu katika kuchapisha vitabu vya sayansi na hisabati kama namna nyingine ya kuchangia jitihada za kuboresha elimu yetu,” Rais Kikwete amemwambia Dkt. Tanaka.
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa hakika, tumekuwa tunapata msaada mkubwa kutoka Serikali ya Marekani katika uchapishaji wa vitabu vya kiada kwa ajili ya shule zetu za sekondari. Lakini bado mahitaji yetu ni makubwa na hivyo tunaomba kama mnaweza mtusaidie katika eneo hili ambalo nalo ni la kuendeleza ubora wa elimu yetu.”
Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kuwa wakati wa mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amekubali kwamba atasaidia katika eneo hili la sayansi na hisabati.
Dk. Tanaka amemwambia Rais Kikwete kuwa JICA inatilia maanani maendeleo ya sekta ya elimu na kuwa kati ya vijana 70 wa kujitolea wa Japan ambao wanapelekwa Tanzania kila mwaka kiasi cha vijana 20 ni walimu wa hisabati na sayansi.
“Tunachoweza kusema ni kwamba tutaangalia kwa makini eneo hili na tutachukua hatua stahiki katika kuwasaidia walimu wa hisabati na sayansi. Aidha, tutaangalia ni kwa namna gani tunaweza kuongeza idadi ya walimu wa hisabati na sayansi miongoni mwa vijana wa kujitolea wanaokwenda kufundisha katika shule za Tanzania kutoka Japan kila mwaka.”