Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesisitiza kuwa Serikali yake haija fikiria kujenga barabara ya lami kukatisha Hifadhi ya Taifa ya Wanyapori ya Serengeti lakini bado Serikali itawapa wananchi wa Loliondo, mkoani Arusha, na Mugumu, mkoani Mara barabara nzuri ya lami.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa watu wanaokejeli umeme unaowaka katika mji wa Loliondo kuwa ni wa jua (solar) ni wanafiki na amewataka wananchi wa mji huo kuwapuuza. Rais Kikwete ameyasema hayo Ijumaa ya Agosti 3, 2012, wakati alipohutubia mamia ya wananchi wa mjini Loliondo na Wasso baada ya kuwa amekabidhi ng’ombe 500 kwa wakazi wa Wilaya ya Ngongoro ambao walipoteza mifugo yao yote kutokana na ukame wa mwaka 2008/09 katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Arusha. Akizungumza na wananchi hao katika eneo la Wasso, Rais Kikwete amesema kuwa ujenzi wa kilomita 50 za kwanza za barabara hiyo inayopitia Loliondo utaanza msimu huu wa fedha kuanzia mjini Mugumu, Mkoani Mara.
“Tumesema na kusema mara nyingi tu kuwa hatukusudii kujenga barabara ya lami kukatisha Hifadhi ya Serengeti lakini tutawapa wananchi wa Loliondo na Mugumu barabara za lami kwa maana ya barabara ya lami kutoka Mto wa Mbu kupitia Loliondo hadi kwenye mlango wa kuingia Hifadhi ya Serengeti upande wa Magharibi na kutoka Mugumu hadi lango la kuingilia Hifadhi ya Serengeti upande wa Mashariki wa Hifadhi hiyo,” amesema Rais Kikwete huku akishangiliwa na wananchi.
Rais Kikwete amesema: “Watanzania wote wana haki sawa ya kupatiwa maendeleo kwa fedha zao wenyewe. Kuna haki gani wananchi wa sehemu nyingine kupatiwa maendeleo kwa fedha za umma, lakini wale wa Loliondo na Mugumu kunyimwa haki hiyo? Waambie hao watu wanaolipwa kusema uongo kuhusu ujenzi wa barabara hiyo waendelee. Wanapotosha ili waendelee
kulipwa. Lakini kwa hili la barabara hatutawasikiliza.”
Kuhusu umeme wa mjini Loliondo, Rais Kikwete amesema kuwa umeme wa Loliondo ni matokeo ya ahadi yake na wanaoukejeli umeme huo wakiuita wa jua (solar) wanakasirika kwa sababu Serikali imetimiza ahadi yake ya kuwapatia wananchi wa wilaya za Ngorongoro na Longido umeme.
“Nasikia wanajekeli umeme, wanasema kuwa eti ni wa solar na kuwa hauwaki vizuri. Watu hawa ni wanafiki tu. Kwao yamekuwa maneno ya kawaida sasa. Yasiwawabaishe. Endeleeni na shughuli zenu,” amesema Rais Kikwete na kuahidi kuwa serikali itaongeza fedha ili kununua nguzo na nyaya zaidi ili kuwezesha majenereta yote manne yaliyofungwa Loliondo kufanya kazi. Kati ya majenereta hayo manne, ni moja tu linafanya kazi ingawa mahitaji ya umeme ni makubwa. Baada ya kumaliza hotuba yake, Rais Kikwete aliamua kwenda kutembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Loliondo kujionea mwenyewe mitambo inavyofanya kazi na kupata maelezo.
Wakati wa sherehe hiyo, ambako Rais Kikwete alikabidhi ng’ombe 64 za mwanzo kwa kaya 16, wananchi wa Wilaya Ngorongoro walimshukuru Rais Kikwete na Serikali yake kwa miradi ya umeme, maji, barabara ya lami, shule za kata na mradi wa kuwawezesha kwa ng’ombe. Kabla ya kuondoka Loliondo kwenda Dodoma, Rais Kikwete ametembelea Hospitali Teule ya Wilaya ya Ngorongoro ya Wasso ambako amewajulia hali wagonjwa kwenye hospitali hiyo.