LICHA ya serikali kuadhimisha wiki ya maziwa Kila mwaka kwa lengo la
kuhamasisha unywaji wa maziwa , hali ya unywaji wa maziwa hapa nchini
bado umetajwa kuendelea kuwa chini ikilinganishwa na nchi nyingine za
jumuiya ya Afrika mashariki.
Unywaji wa maziwa katika nchi ya Tanzania kwa sasa ni Lita 44 kwa mtu
mmoja kwa mwaka wakati shirika la Afya duniani (WHO) na shirika la
Chakula (FAO)wamependekeza unywaji wa maziwa ufikie angalau Lita 200
kwa mtu kwa mwaka.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya 15 ya wiki ya maziwa
na Kongamano la Tisa la kuendeleza Tasnia ya Maziwa hapa nchini
inayofanyikia mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, mratibu wa mradi wa
uendelezaji tasnia ya maziwa Tanzania (EADD) ulioko chini ya Bill and
Melinda Gates, Dkt. Aichi Kitalyi alisema katika nchi ya Tanzania
unywaji wa maziwa bado uko chini sana ikilinganishwa nchi nyingine
kama Kenya,Uganda na Rwanda kutokana na kukosekana kwa mwamko wa
ufugaji Ng’ombe wa maziwa ambapo wananchi wengi hufuga Ng’ombe wa
nyama.
Dkt. Kitalyi alisema wakati nchi ya Tanzania wastani wa unywaji
maziwa ukiwa lita 44 kwa mtu kwa mwaka nchini Kenya unywaji wa maziwa
ni Lita 120 huku nchini Uganda ikiwa ni zaidi ya Lita 80 kwa mtu kwa
mwaka na kwamba uzalishaji nao ni duni ikilinganishwa na nchi za hizo
za jumuiya ya Afrika mashariki hali ambayo inasababishwa na
kukosekana kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa vyakula vya ziada vya
mifugo pamoja na kutokuwepo kwa ng’ombe sahihi wa maziwa.
Alisema wapo waandaaji wa chakula cha ziada cha mifugo ambao
hutengeneza chakula kisicho na kiwango ambapo wapo ambao husaga
magunzi na kuchanganya na pumba na mfugaji anaponunua anaona ni
chakula kizuri cha kuongeza uzalishaji wa maziwa jambo ambalo si
sahihi.
“kwa kweli unywaji wa maziwa hapa nchini kwetu bado uko chini sana na
kutokana na hali ya maendeleo sasa tunapaswa kuongeza unywaji wa
maziwa lakini si unywaji tu pia uzalishaji wa maziwa kwani nao uko
chini”alisema Dkt. Kitalyi.
Akizungumza meneja wa mradi wa uendelezaji tasnia ya maziwa Afrika
mashariki (EADD) Bi. Alice Makochieng alisema katika nchi za afrika
mashariki maziwa ni mengi lakini katika kipindi cha kiangazi hupungua
sana na ni kutokana na kutojiandaa katika kukabiliana na hali ya
kiangazi na kwamba kwa sasa wamejipanga kuongeza uzalishaji na unywaji
wa maziwa nchini Tanzania kwani hawataki iendelee kubaki nyuma.
Naye mkurugenzi msaidizi uendelezaji wa mazao ya mifugo kutoka katika
sekta ya Mifugo Dkt. Yacob Masanga alisema kwa sasa wanampango wa
kuhamasisha unywaji wa maziwa hapa nchini ili kuweza kufikia wastani
wa lita 200 kwa mtu kwa mwaka.
Akifungua maadhimisho hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro
Bw. Leonidas Gama, kaimu katibu tawala wa mkoa huo Bi. Ruth Malisa
alisema suala la Unywaji wa maziwa hapa nchini ni changamoto kubwa
inayohitajika kushughulikiwa kutokana na kwamba bado uko chini sana
ikilinganishwa na nchi nyingine licha ya kuwepo kwa fursa nyingi za
kuendeleza sekta ndogo ya Maziwa.
Alisema katika mkoa wa Kilimanjaro wastani wa unywaji wa maziwa ni
Lita Sita kwa mtu kwa mwaka na kwamba mkoa huo una fursa zaidi
katika kuendeleza tasnia ya maziwa kwa kuwa na hali ya hewa nzuri.
Akizungumzia uzalishaji wa maziwa Bi. Malisa alisema nao uko chini
ambapo kwa mwaka hapa nchini huzalishwa maziwa Lita Bil. 1.74
kutokana na Ng’ombe 720,000 wa maziwa na kwamba viwanda vya kusindika
maziwa hapa nchini vinauwezo wa kusindika Lita 410,000 kwa siku
lakini kwa sasa vinasindika lita 112,400 kwa siku.
Wiki ya maziwa ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia May 29 hadi jun
mosi kwa mwaka huu inaadhimishiwa mkoani Kilimanjaro ikiwa na kauli
mbiu isemayo, ‘kuza uchumi na Lishe,Fanya maziwa kuwa moja kati ya
mazao makuu ya wilaya.