RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Ujerumani kwa kutwaa Kombe la Dunia mwaka huu. Rais Kikwete ametoa pongezi hizo kwa Balozi mpya wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mheshimiwa Egon Kochanke ambaye amewasilisha Hati zake za Utambulisho leo asubuhi Ikulu .
“Naipongeza Ujerumani kwa kuibuka washindi natumaini tutashirikiana vyema katika masuala ya utamaduni hasa hasa katika kuinua kiwango cha soka nchini Tanzania na kuzisaidia klabu za Tanzania kuanzisha shule maalum kwa ajili ya mpira wa miguu nchini.” Rais amesema na kuishukuru Ujerumani kwa misaada mbalimbali katika sekta za Maji, Utalii, Usafiri wa majini na maeneo mengine ya maendeleo.
Rais pia amepokea Hati za Mabalozi Richard Stuart Man wa New Zealand na Bw. Claude Morel wa Ushelisheli ambao wana makazi yao Pretoria, Afrika ya Kusini na Balozi Sander Kocsis wa Hungary mwenye makazi yake Nairobi , Kenya.
Baadae leo mchana, Rais Kikwete amekabidhi Bendera ya Taifa kwa Timu ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, inayotarajiwa kufanyika Glasgow kuanzia tarehe 23 Julai hadi tarehe 3 Agasti mwaka huu.
Hafla ya kuiaga Timu hiyo imefanyika katika Uwanja wa Taifa jijini na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard Membe na Naibu waziri, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia.
Timu ya Tanzania inatarajiwa kuondoka kesho tarehe 16 Julai,2014 kuelekea Scotland ambapo inatarajiwa kushiriki katika Riadha, Ngumi, Mpira wa Meza, Judo, Kuogelea, Baiskeli na Kunyanyua vitu vizito.
Rais amewaambia washiriki waende wakijua kuwa wana deni la kutunza heshima binafsi kama wachezaji na heshima ya Nchi na Taifa kwa ujumla.
“Siri ya mafanikio ni maandalizi mazuri na tumewekeza sana kwenye mafunzo na maandalizi yenu na hivyo safari hii maandalizi yalikuwa mazuri, hivyo mna deni kubwa” Rais amesema.