Tanzania Yaionya Malawi Kuhusu Mgogoro wa Mpaka

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (wapili kutoka kulia) akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu tamko la Serikali juu ya mgogoro wa mpaka wa ziwa Nyasa. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, John Haule.


Na Benedict Liwenga, Johary Kachwamba na Magreth Kinabo – MAELEZO

SERIKALI ya Tanzania imeitaka nchi ya Malawi iache kutapa tapa juu ya mgogoro wa mipaka wa Ziwa Nyasa kufuatia Rais wa nchi hiyo, Joyce Banda kutangaza katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa atapeleka suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), badala yake isubiri uamuzi wa jopo la usuluhishi lifanye kazi na litoe maamuzi.

Aidha serikali imesema kuwa hata siku moja haijapelekewa taarifa wala nyaraka za siri kutoka kwa Katibu wa jopo hilo, ambalo linahusisha marais wastaafu wa zamani wa Afrika na wanasheria kama ilivyodaiwa na Rais Banda katika vyombo hivyo, kuwa kuna Mtanzania anayeitwa Dk. John Tesha ambaye wanaamini ametoa habari na kuiba nyaraka za siri.

Akilitolea ufafanuzi jambo hili, Waziri Membe amesema kuwa Tanzania na jopo hilo limestushwa juu ya madai hayo na hatua ya Rais Banda kupoteza imani. Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati akizungumzia na waandishi wa habari juu ya mgogoro huu kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara jijini Dares Salaam.

Kwa kuwa baada ya kuwasilisha barua na nyaraka zake Dk. Tesha hatahusika katika suala hilo ili kuondoa uwezekano wa nchi hiyo (wenzetu) kulalamika. Pia hata marais wastaaafu kutoka katika nchi zenye migogoro ya mipaka hawatahusika kwa sababu ya kuzuia ‘confilict of interest’.

“Serikali ya Tanzania ina imani na jopo linaloongizwa na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano na marais wengine ambao ni Festus Mogae na Thabo Mbeki, kwa kuwa lina watu wenye uzoefu, wataalamu na wachapakazi. Pia kuna jopo la wanasheria na wataalamu wa masuala ya migogoro limeundwa na ni la watu saba,” alisisitiza Waziri Membe.

Aliwataja wanasheria hao kuwa ni Jaji Raymond Ranjeva, ambaye ni Jaji mstaafu wa ICJ, Profesa George Kanyeihamba (Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Uganda, Jaji Baney Afako (Mshauri wa masuala ya sheria kwenye Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan), Dk. Gbanga Oduntun(Profesa wa Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa mpaka kati ya Nigeria na Cameroon).

Wengine ni Profesa Martin Pratt, (ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Geografia na Mipaka), Dk. Dire David Tladi (Mjumbe wa Kamisheni ya Sheria ya Umoja wa Mataifa) na Miguel Chisano(Kiongozi wa Chuo kinachoshughulikia mipaka ya Baharini na Nchi Kavu.

“Ni watu wenye heshima ya dunia tusingetegemea…kusema hana imani na jopo hili,” alisema.
Akirejea mazungumzo ya makubaliano yaliyofanyika Novemba 17, mwaka (2012) kuwa walikubaliana hapo walipo katika jopo hilo ndipo sehemu ya mwisho. Hivyo wataenda ICJ iwapo watashauriwa na jopo la mzee Chissano.
“Wakati tunasubiri jopo kufanya kazi na kutoa majibu Serikali inaiomba Malawi pale katikati ya Ziwa Nyasa pasiguswe mpaka jibu litakapotolewa na jopo la usuluhishi. Tunaiomba serikali ya Malawi irudi katika jopo la usuluhishi na tutashangaa ikiwa Malawi itakwenda kushtaki ICJ kwa kuwa ili Malawi iende ICJ ni lazima sisi tukubali. Hata pale tutakaposhauriwa ni lazima sisi tukubaliane na Malawi,” alisisitiza Waziri Membe.

Hivyo aliiomba Serikali ya Malawi iache kutapatapa mara Uingereza, Marekani, Jumuia ya Madola na Umoja wa Afrika (AU) na kuona viongozi mbalimbali wa dunia, bali iamini jopo la Mzee Chissano. Matokeo ya utafiti wao upo uwezekano wa kuyakubali au kuyakataa.

Akizungumzia kuhusu utoaji wa ripoti ya jopo hilo utakuwa ni lini,Waziri Membe alisema Tanzania haina haraka juu ya jambo hilo. Waziri Membe alisema Tanzania, ilipeleka wataalamu Uingereza na Ujerumani ili kupata uelewa wa kutosha juu ya jambo hilo, hivyo ina ushahidi wa kutosha.